Monday, January 29, 2018

JAFO APIGA MARUFUKU UJENZI WA MADARASA YA UDONGO AU TEMBE

Seleman Jafo.
Na Lilian Lundo,
Maelezo Dodoma.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Seleman Jafo amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halamshauri zote nchini, kuhakikisha kwamba wanajenga madarasa yenye ubora na viwango vinavyokubalika ili kuondokana na tatizo la baadhi ya Wilaya kuwa na majengo ya udongo au tembe.

Jafo alitoa agizo hilo leo mjini Dodoma alipokuwa akifungua mafunzo ya uongozi ya siku tano kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi toka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara yanayoendelea kufanyika katika ukumbi wa Hazina Mkoani humo.

“Sitaki kuona madarasa ya udongo, tembe na watoto kusomea nje hakikisheni matumizi ya mapato ya ndani yanagusa na kujibu matatizo ya wananchi”, alisisitiza Jafo.


Waziri Jafo aliwataka Wakuu wa Wilaya kuhakikisha kwamba matumizi ya mapato ya ndani katika Halmashauri zao, yanatumika katika miradi mbalimbali ya wananchi ikiwemo ujenzi wa madarasa ili kuondokana na uwepo wa madarasa ya udongo na tembe katika Halmashauri zote hapa nchini.

Aidha aliwataka Wakurugenzi wa Halmashauri kufanya maamuzi ya haraka mara wanapopokea fedha za miradi ya maendeleo, kauli hii imetokana na baadhi ya Wakurugenzi kuwa wazembe katika kufanya maamuzi hivyo kuchelewesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya zao na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Naibu Waziri TAMISEMI Josephat Kandege naye alisema anaamini Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi hao wataenda kutekeleza yale ambayo watajifunza katika mafunzo hayo.

“Naamini kwa fursa hii ya mafunzo haya mtakuwa vinara mara mbili au tatu ya mlivyokuwa katika kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)”, alisema Kandege.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa taasisi ya uongozi Profesa Joseph Semboja alifafanua kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuimarisha uwezo wa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri katika kufanya maamuzi ya kimkakati, kuwapa uwezo wa kuongoza watu na rasilimali nyingine pamoja na kuimarisha uwezo wao katika sifa zao binafsi.

Profesa Semboja alisema awamu hii ya nne ya mafunzo ya uongozi kwa viongozi hao inakamilisha idadi ya viongozi 324 wa Wilaya na Mamlaka ya Serikali za Mitaa waliotarajiwa kupata mafunzo hayo kwa nchi nzima.


Mafunzo ya uongozi kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri yalizinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Mei 9 mwaka jana ambapo yameendeshwa kwa awamu tatu tofauti na awamu hii ya nne ndiyo awamu ya mwisho inayofunga mafunzo hayo kwa viongozi hao wa Wilaya na Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

No comments: