Sunday, January 7, 2018

SERIKALI KUKIFANYA KITUO CHA LILAMBO SONGEA KUWA KITUO KIKUU CHA UNUNUZI MAZAO

Na Muhidin Amri,      
Songea.

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema, Serikali itaangalia uwezekano wa kukifanya kituo cha kuongeza thamani ya mazao kilichopo katika eneo la Lilambo kata ya Ruhuwiko Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, kuwa kituo kikuu cha ununuzi na uuzaji wa mazao.

Majaliwa alisema hayo juzi wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Lipokela kata ya Lipokela wilayani Songea, baada ya kukagua mradi mkubwa wa shamba la kahawa ambalo linamilikiwa na Kampuni ya AVIV Tanzania Limited.

Alisema kuwa Mkoa huo ni kati ya mikoa saba hapa nchini ambayo inaongoza kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali na kwamba Serikali kuanzia msimu ujao itatekeleza hilo ili mazao yanayolimwa mkoani humo yaweze kupata soko na kuwaondolea umaskini wakulima.


"Nakubaliana na maombi ya Mbunge wa jimbo la Peramiho Jenista Mhagama kuwa kituo hiki kitumike hata kwa kuuzia na kununua mazao ya wakulima, mkoa huu umekuwa ukifanya vizuri katika uzalishaji wa mazao mbalimbali", alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Aidha amewataka wakulima wa Mkoa wa Ruvuma kuongeza juhudi katika kilimo hasa wakati huu ambao Serikali nayo inahangaika kutafuta masoko kwa ajili yao, kwa kuwa  kilimo ni kati ya vyanzo vikubwa vinavyoingiza mapato. 

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu huyo alisema kuwa Mkoa  huo pia ni wa kwanza hapa nchini ambao unalima karibu mazao yote makubwa ya biashara yanayochangia kukua kwa uchumi wa nchi ambayo ni korosho, kahawa, tumbaku na mahindi.

Katika hatua nyingine aliwahimiza wakulima wa wilaya ya Songea kwa kuwataka kuanzia sasa kulima zao la kahawa ambalo lina faida kubwa ikilinganishwa na mazao mengine hasa kutokana na hali ya hewa ya Songea kuwa rafiki wa zao hilo.

Awali Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, sera, bunge, uratibu na wenye ulemavu ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Peramiho Jenista Mhagama aliiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuongeza ununuzi wa mahindi yaliyozalishwa na wakulima wa mkoa wa Ruvuma ambayo bado wanayo majumbani kwao.

Mhagama alisema katika msimu wa kilimo wa 2016/2017 wakulima wa mkoa huo waliweza kuzalisha mahindi tani laki 8.78 lakini kiasi kilichonunuliwa na Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifahdi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Songea ni tani 300 huku wakulima wakiwa na mahindi mengi majumbani.

Kadhalika alimuomba Waziri Mkuu kukifanya kituo cha kuongeza thamani mazao cha Lilambo katika Manispaa ya Songea kuwa ndiyo kituo kikuu cha biashara ya mazao ya wakulima hasa mahindi katika Mkoa huo.

No comments: