Wednesday, January 17, 2018

HALMASHAURI MJI WA MBINGA WATAKIWA KUPANDA MITI RAFIKI YA MAJI



Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

WANANCHI wanaoishi katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma, wametakiwa kuendelea kupanda miti rafiki ya maji kwa wingi hasa kipindi hiki ambacho ni cha mvua za masika katika maeneo yenye vyanzo vya maji, ili kuweza kuondokana na tatizo la upungufu wa maji katika kipindi cha kiangazi.

Mwito huo umetolewa jana na Meneja wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (MBIUWASA) katika Mji huo, Patrick Ndunguru wakati wa zoezi ambalo mamlaka hiyo inaendelea nalo la upandaji miti kuzunguka vyanzo mbalimbali vya maji ndani ya mji huo.

“Mkakati tulionao wa mamlaka hii ni kurudisha uoto wa asili katika vyanzo vya maji ambavyo vimeanza kupotea kutokana na baadhi ya wananchi kuendesha shughuli zao ikiwemo kilimo”, alisema.


Ndunguru alisema kuwa sababu kubwa ya uharibifu wa mazingira hayo imejitokeza hasa kutokana na wananchi hao kupendelea kulima kilimo cha bustani kando kando ya mito na kwenye vyanzo vingine vya maji.

Kadhalika Meneja huyo wa MBIUWASA amewataka viongozi wa vijiji na mitaa washirikiane na mamlaka hiyo kuhakikisha kwamba wanakemea hali hiyo na kuwachukulia hatua watu wanaokiuka suala la utunzaji wa mazingira hasa kwa wale wanaoendesha shughuli za kilimo kwenye vyanzo hivyo ili kuweza kudhibiti uwezekano wa kupungua kwa maji katika Mji wa Mbinga.

Vilevile ameishukuru Serikali kwa uamuzi wake uliotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa juu ya kuzuia ujenzi wa Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga katika eneo la chanzo cha maji Ndengu ambalo ndiyo tegemeo kwa kuzalisha na kulisha maji wakazi wa Mji huo.

“Kwa kweli Serikali imefanya jambo la maana sana, kwetu sisi kama mamlaka kuzuia ujenzi wa Ofisi pale katika eneo la Ndengu endapo ingeruhusu basi kungetokea madhara makubwa ambayo hapo baadaye wananchi wangetumia maji ambayo sio salama kwa maisha yao”, alisema Ndunguru.

Awali katika kipindi cha mwaka jana, kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kilipitisha uamuzi wake wa kujenga Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo katika kijiji cha Ndengu kata ya Nyoni baada ya kugawanywa na kuanzishwa Halmashauri ya Mji wa Mbinga.

Hata hivyo imeelezwa kuwa Wajumbe wa kikao hicho licha ya kupitisha maamuzi hayo hawakutambua umuhimu wa eneo hilo na athari zinazoweza kujitokeza hapo baadaye kwa kujenga Ofisi na makazi ya watumishi katika eneo hilo ambalo limehifadhiwa kwa ajili ya vyanzo vya maji.

No comments: