Monday, May 7, 2018

WAKULIMA WASHAURIWA KUJENGA MAHUSIANO NA VIONGOZI WA SERIKALI

Wakulima wa kahawa Mbinga wakipeana mawazo namna ya kuzingatia kanuni bora za uendeshaji wa vyama vyao vya ushirika.

Na Mwandishi wetu,      
Mbinga.

VIONGOZI waliopo katika Vyama vya ushirika wa kahawa Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma, wamesisitizwa kujenga mahusiano mazuri na viongozi wa Serikali ambao wamepewa dhamana ya kusimamia maendeleo ya vyama hivyo Wilayani humo, ili kuweza kuvifanya viweze kusonga mbele kimaendeleo.

Aidha imeelezwa kuwa ushirika wa zao hilo katika maeneo mbalimbali ndani ya Wilaya hiyo ulifikia hatua ya kufa, kutokana na utendaji mbaya na kutokuwepo kwa ushirikiano mzuri kati ya wakulima na viongozi hao.

Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na viongozi wa vyama vya ushirika katika mafunzo elekezi yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mbicu hotel uliopo mjini hapa.


“Ndugu zangu ushirika ni sehemu ya Serikali hivyo nasisitiza juu ya uwepo wa mahusiano mazuri katika utendaji wenu wa kazi, ninyi viongozi mkiona wakulima wanadhulumiwa mnapaswa kuvaa ile sura ya uadilifu na kutenda haki kwa hiyo suala hili la uadilifu nawataka huko muendako mkalizingatie”, alisisitiza Nshenye.

Nshenye amewataka pia wabadilike na kuachana na vitendo vya wizi na kwamba ameapa kuwa pale atakaposikia kiongozi yeyote yule wa chama cha ushirika Wilayani hapa amehusika kumuibia mkulima Serikali itachukua hatua kali za kisheria ikiwemo kumfikisha Mahakamani.

Alifafanua kuwa viongozi hao wa vyama vya ushirika wanapaswa kuweka wazi utendaji wao wa kazi ikiwemo bei na taarifa za mauzo ya kahawa zao na sio kutengeneza mbinu za kificho.

Naye Benigna Haulle ambaye ni Mratibu wa mafunzo hayo kutoka chuo kikuu cha ushirika Moshi Ofisi ya Mkoa wa Ruvuma, alisema kuwa mpango uliowekwa na Serikali hivi sasa ni kutaka kuona mkulima anayezalisha kahawa ananufaika na zao lake na sio vinginevyo.

Haulle alibainisha kuwa Halmashauri za Wilaya zinapaswa kudhibiti ubora wa kahawa kwa kushirikiana na wakulima wenyewe na kwamba hivi sasa Makampuni yatanunua kahawa mnadani lakini vyama vyote vya ushirika vinapaswa kuomba kibali cha kununua zao hili katika halmashauri husika.

“Kila mmoja wetu achukue nafasi hii kuwajibika ipasavyo hebu sasa tuvae kikamilifu sura ya mkulima, tuachane na vitendo vya hujuma ambavyo hurudisha nyuma maendeleo ya mkulima”, alisema Haulle.

Kwa upande wake Leo Kumburu ambaye ni Afisa kilimo wa Wilaya ya Mbinga kitengo cha ukaguzi na ubora wa kahawa aliwataka wakulima wa zao hilo kuachana na vitendo vya kuanika kahawa mbivu chini badala yake wanapaswa kuanika kwenye meza maalum ili kuweza kulinda ubora wake.

Vilevile alipiga marufuku biashara za magoma ya kahawa huku akitaka kahawa yote inayopokelewa kwenye chama husika cha ushirika ipokelewe kwa stakabadhi maalum.

No comments: