Na Julius Konala,
Songea.
MFUKO wa Taifa Bima ya Afya (NHIF) mkoani Ruvuma, umevuna
wanachama zaidi ya 100 wa chama cha ushirika wa akiba na mikopo Mahanje SACCOS
waliopo katika Halmashauri ya Madaba wilayani Songea mkoani humo baada ya kujiunga
na mfuko huo.
Wanachama hao wamejiunga na NHIF baada ya kuhamasika na
maelezo yaliyotolewa na Ofisa wanachama wa mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya mkoa
wa Ruvuma, Anthony Mgina alipopewa nafasi ya kuelezea faida za mfuko huo katika
mkutano mkuu wa 19 wa chama hicho uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa
Tumaini Madaba uliopo mjini hapa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wetu, wanachama
hao walisema kuwa wameamua kujiunga na mfuko huo kwa lengo la kupata huduma mbalimbali
za matibabu kwa urahisi pamoja na kupunguza pia gharama za matibabu hayo.
Wanachama hao walidai kuwa wananchi wengi wamekuwa
wakikabiliwa na tatizo kubwa la kushindwa kumudu gharama za matibabu, kwa kushindwa
kujiunga na mfuko huo.