Na Bashir Yakub,
TULIPOANDIKA namna bora na taratibu
maalum za kufuata unapotaka kununua ardhi,
tulisema pia taratibu za ununuzi wa ardhi
huwa zinatofautiana kutegemea na mazingira
ya kila ardhi. Tukasema unaponunua ardhi
kwa msimamizi wa mirathi, ni tofauti
na unaponunua kwa mmiliki mwenyewe.
Unaponunua ardhi ya familia ni
tofauti na unaponunua isiyo ya familia.
Vilevile unaponunua ardhi ya kijiji ni
tofauti na unaponunua ardhi isiyo ya kijiji. Taratibu
hutofautiana na hasa tofauti ipo katika
nyaraka ambazo zinatakiwa kuambatanishwa, ikiwa
kama ithibati ya ununuzi. Hata uandishi
wa mkataba wa manunuzi pia nao huwa na
tofauti katika hili.
1. ARDHI YA KIJIJI KWA UWEKEZAJI.
Wako watu wamekuwa wakinunua
ardhi hasa huko vijijini, lakini baadae
wamekuwa wakijikuta katika migogoro mikubwa
na wenyeji. Mwamko wa kununua maeneo kama
Bagamoyo, Kisarawe, huko Chanika Dondwe na maeneo
mengine umekuwa mkubwa sana. Hata hivyo
mwamko unavyoongezeka ndivyo na migogoro
inavyoongezeka. Kubwa katika migogoro hii ni
hatua ya wanunuzi kutokufuata utaratibu wa
ununuzi aidha kwa kujua, kutokujua au kupotoshwa.
Wakati mwingine ni uelewa mdogo
miongoni mwa wenyeji, lakini zaidi ni
hili la kutofuata utaratibu. Mara zote huwa
tunasema ni bora zaidi mgogoro unapotokea halafu
ukukute ulifuata taratibu wakati wa manunuzi.
Bila shaka hautakuwa na athari kubwa kwako,
lakini ni mbaya zaidi ukitokea halafu
ukukute kuna taratibu hukufuata kwa bahati mbaya
au bila kujua. Unakuwa katika hatari ya kupoteza.
Unapokwenda kununua ardhi ya kijiji
kwasababu yoyote ile hasa uwekezaji, upo
utaratibu maalum wa kufuata nitakaoeleza.