Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, mtu mmoja ambaye ni mkazi wa
kijiji cha Zomba wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Dickson Lupogo (28) ameuawa
kikatili kwa kushushiwa kipigo kikali na baadaye mwili wake kuchomwa moto na
watu wenye hasira kali, baada ya kufanya mauaji ya watoto wawili na kumjeruhi
mmoja.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela. |
Mwandishi wa habari hizi ambaye aliwasili eneo la tukio,
majira ya asubuhi leo Novemba 15 mwaka huu, alishuhudia mauaji hayo
yaliyofanyika katika mtaa wa Tangi la maji A Mbinga mjini na kuelezwa kwamba,
Lupogo alifanyiwa unyama huo kutokana na kitendo chake cha kuwaua
kikatili watoto hao na mmoja kumjeruhi vibaya.
Kadhalika Adrian Ndunguru ambaye ni mjomba wa Lupogo, alisema
kuwa marahemu huyo alifanya mauaji hayo Januari 14 mwaka huu, majira ya usiku
ambapo alienda nyumbani kwa Paulo Ndunguru katika mtaa huo wa Tangi la maji na kumweleza kwamba hawezi kurudi kijijini kwao Zomba, badala yake
atalala hapo au ampeleke Polisi kwa maelezo kwamba akihofia atauawa endapo kama
angerejea nyumbani kwake.
Adrian alifafanua kuwa baada ya kupokea maelezo hayo, Paulo hakukubaliana
na wazo lake kwakuwa hakutoa ufafanuzi wa kina, badala yake alimwacha pale
nyumbani na kwenda kwa mama yake marahemu Dickson Lupogo, anayeishi mtaa wa Masumuni jirani
mjini hapa, kwa lengo la kushauriana naye juu ya maelezo hayo yaliyotolewa na mtoto
wake.
Kwa upande wake akielezea tukio hilo, Paulo alisema kuwa
wakati akiwa njiani kuelekea kwa dada yake, ghafla alipigiwa simu na mke wake
Adella Mhagama akielezwa kwamba mjomba wake ambaye ni Lupogo, alikuwa akiwapiga
watoto waliokuwa wamelala chumbani kwao.
Alisema baada ya kufika nyumbani kabla ya kuingia ndani
alikutana na Dickson ambaye alimvamia ghafla huku akiwa ameshika kisu mkononi,
na ndipo alipambana naye huku akipiga kelele akiomba msaada ambapo majirani
waliwasili na kumkamata asiweze kuleta madhara, huku wakimfunga kamba miguu na
mikono.
Baada ya tukio la kufungwa kamba, walipoingia ndani walikuta
watoto watatu kati yao wawili wakiwa wameuawa na mmoja akiwa amejeruhiwa vibaya,
pembeni yake pakiwa na chuma kizito chenye damu, ambacho kinadaiwa kutumika
katika mauaji ya watoto hao.
Kugundulika kuuawa kwa watoto hao, ndiko kulizua hasira na walipotoka
nje ndipo walimpiga vibaya mtuhumiwa aliyefanya ukatili huo wa kinyama na
baadaye alichomwa moto majira ya saa 5:00 usiku, huku mwili wake ukiteketezwa
baadhi ya maeneo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataja marehemu kuwa ni watoto wawili,
Lulu Chang’a (14) na Furaha Ndunguru (7) ambaye ni wa darasa la kwanza shule ya
msingi Nyerere iliyopo Mbinga mjini.
Msikhela alifafanua kuwa mtoto Moses Ndunguru (3) amejeruhiwa
vibaya na amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Mbinga, ambako anaendelea na
matibabu na hali yake ni mbaya, na kwamba miili ya marehemu hao inatarajiwa
kuzikwa leo nyumbani kwao mjini hapa.
Pamoja na mambo mengine, Kamanda huyo wa Polisi aliongeza
kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo ili
kuweza kubaini chanzo chake na kutoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma,
kuacha tabia ya kuchukua sheria mkononi badala yake watoe taarifa kwenye vymbo
vya kisheria ikiwemo Polisi.
Hata hivyo Daktari Mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Mbinga,
Dokta Robert Elisha alisema kuwa miili ya marehemu hao imejeruhiwa vibaya
kutokana na kupigwa na kitu kizito kichwani, kitendo ambacho kilisababisha
kutokwa na damu nyingi na kwamba kwa upande wa mtoto aliyejeruhiwa, Moses
Ndunguru ana majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake na kwamba kutokana na
hali yake kuwa mbaya, huenda akapelekwa Hospitali ya misheni Peramiho iliyopo
wilaya ya Songea au Litembo hapa mkoani Ruvuma kwa matibabu zaidi.
No comments:
Post a Comment