Na Bashir Yakub,
NILIWAHI kuandika kuwa, mkopo sawa
lakini haki za mkopaji zilindwe. Nikasisitiza
kuwa kushindwa kurejesha mkopo wote au
sehemu yake hakuondoi haki za kisheria
alizonazo mkopaji. Katika hilo nilizungumzia
taratibu mahsusi za kisheria zinazotakiwa
kufuatwa wakati taasisi ya fedha inapofikia
uamuzi wa kuuza dhamana ya mkopaji, nyumba au kiwanja.
Mara nyingi ukiukwaji wa haki za
mkopaji hutendwa na taasisi iliyotoa mkopo
au kampuni za udalali (brokers) ambazo hupewa
kazi ya kunadisha mali ya mkopaji.
Wakati mwingine yawezekana kabisa taasisi
ya fedha ikawa imefuata taratibu zote za
kisheria, lakini tatizo likajitokeza kwa dalali
(brokers) aliyepewa kazi ya mnada. Na hivyo
ndivyo ambavyo imekuwa ikijitokeza na hiyo
ni kwasababu moja tu, kwamba hupenda
kujipatia faida kubwa na ya haraka katika
mali inayonadishwa. Ni katika kufanya hivyo hujikuta
wamekiuka haki na taratibu za uuzaji kwa
ujumla. Kwa ufupi haki na wajibu
ni vitu vya kuzingatia sana katika miamala
ya mkopo, hasa ikizingatiwa kuwa jambo
hilo huhusisha fedha na mali kama nyumba
ambamo wakati mwingine ndimo yalimo makazi
yetu.
1.WAJIBU WA MTOA MKOPO.
Sheria ya rehani ya mwaka 2008
imeeleza vizuri baadhi ya wajibu walionao
watoa mkopo. Tutaangalia baadhi.
( a ) Kwanza kabisa ni wajibu wa mtoa
mkopo kuhakikisha anatafiti na kujua iwapo
mtu anayechukua mkopo ana mke au mume. Hii
ni kwa mujibu wa sheria ikiwa nyumba
au kiwanja kinachowekwa rehani ili
kupata mkopo ni cha familia, kwa
maana cha wanandoa basi ni lazima
wanandoa wote wawe wameridhia na wote kwa
pamoja watasaini waraka maalum kuthibitisha
ridhaa zao. Ikiwa taasisi ya mkopo
haikufanya utafiti na kujiridhisha na hili
basi madhara yatakayopatikana yatawaathiri wao
kwakuwa utakuwa ni uzembe kwa upande
wao. Hairuhusiwi mwanandoa mmoja kutumia mali
ya familia kama dhamana bila ridhaa
ya mwingine.
( b ) Pia mtoa mkopo ana wajibu mwingine
wa kuhakikisha mali inayowekwa kwake kama
rehani haijawekwa rehani sehemu nyingine
yoyote, haina mgogoro wowote katika Mahakama
yoyote ya sheria, haina zuio lolote (caveat) na wala
si ardhi ambayo iko katika mpango fulani wa
serikali ambao utatekelezwa muda mfupi kabla
ya deni kuisha au hapo baadae kidogo. Hii
humuepusha mtoa mkopo kutoingia katika mgogoro
na mamlaka nyingine hasa za serikali
au watu binafsi, ambao wanaweza kuwa na
maslahi katika ile ardhi kabla yake.
( d ) Wajibu mwingine muhimu ni kuhakikisha
wanamweleza mchukua mkopo hali halisi
kuhusu huo mkopo, ikiwa ni pamoja na
athari zake atakaposhindwa kulipa, taratibu za
marejesho, uhuru wa kuongeza mkopo na ukomo,
na kila kitu ambacho ni sehemu ya
muamala wa mkopo.
2. HAKI ZA MCHUKUA MKOPO/MKOPAJI.
( a ) Iwapo kuna badiliko lolote katika
taratibu za ulipaji deni husika, riba yake
au mabadiliko yoyote katika tarehe ya
marejesho ni haki ya mchukua mkopo
kujulishwa kwa maandishi maalum. Taasisi kubwa
za fedha zimekuwa zikilitekeleza hili tofauti
na taasisi ndogo ambazo ndio nyingi
kwa sasa. Katika taasisi ndogo isikushangaze siku
ya kurejesha mkopo ukaambiwa kuwa deni
limeongezeka kwasababu hii na hii na
hivyo hii pesa uliyoleta haitoshi. Wanakiuka
sana haki za wakopaji.
( b ) Ardhi iliyowekwa rehani inaendelea kuwa
haki ya mchukua mkopo ikiwa yule aliyenunua
ardhi hiyo kwa njia ya mnada hajamalizia
hela ya malipo ya mnada kama ilivyokubaliwa.
Wako watu huweza kulipa 25% tu wakati wa
mnada na kushindwa kumalizia salio. Hii
ikitokea maana yake ni kuwa umiliki
bado unakuwa kwa mchukua mkopo na muda
wowote humo katikati anaweza kutafuta hela au
kufanya vinginevyo kukomboa nyumba yake.
( c ) Haki ya kupewa taarifa ya siku
sitini kabla ya mauzo ni haki ambayo
huwa nairejea mara kwa mara kutokana na
umuhimu wake . Si tu kutokana na umuhimu
wake bali pia kutokana na namna ambavyo
huwa haizingatiwi na wengi hasa wanadishaji (brokers).
( d ) Mkopaji ana haki ya kulipa rejesho
na riba kwa viwango vya fedha
vinavyotambulika na kukubaliwa kisheria. Baadhi
ya taasisi fedha hasa zile ndogo zimekuwa
zikijipangia viwango vya marejesho na
riba ambazo ni kubwa kupita kiasi
huku zikiwa zimekiuka taratibu za viwango vya
fedha. Hii ni pamoja kuongeza viwango
hivyo kinyemela huku wakilenga kujipatia
faida kubwa .
Kwa leo ni hayo.
MWANDISHI WA MAKALA
HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA
HABARI LEO KILA JUMANNE, GAZETI
JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI
NIPASHE KILA JUMATANO.
0784482959,
0714047241
bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment