Monday, November 2, 2015

UKAWA RUVUMA YAANGUKIA PUA YASHINDWA KUTAMBA MBELE YA CCM



Na Steven Augustino,
Ruvuma.

WAGOMBEA ubunge katika majimbo tisa kupitia  vyama vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi (UKAWA) mkoani Ruvuma, wameangukia pua na kushindwa kufurukuta kwa wagombea wa nafasi hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kushindwa vibaya katika matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Kufuatia  hali hiyo mkoa huo, umeendelea kubaki kuwa ngome kubwa ya CCM kwani hata katika kura za urais mgombea wake, Dokta John Magufuli ameibuka kidedea kwa kumshinda mpinzani wake, Edward Lowassa wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye aligombea kupitia  UKAWA.

Katika wilaya ya Tunduru yenye majimbo mawili ya uchaguzi, Mbunge wa jimbo la Tunduru Kaskazini, Mhandisi  Ramo Makani alifanikiwa kutetea nafasi yake baada ya kupata kura 29,841 dhidi ya kura 29,102 alizopata mgombea wa Chama Cha Wananchi CUF, Manjolo Kambili huku mgombea wa ACT wazalendo, Mohamed Khalifa akiambulia kura 838.


Pia katika jimbo la Tunduru Kusini, mfanyabiashara maarufu na kada wa CCM Daimu Mpakate alimpeleka puta mgombea wa CUF, Sadick Songoni katika kinyang’anyiro hicho baada ya kumbwaga kwa kura  27,486 dhidi ya kura 16,621 alizopata mgombea huyo wa CUF, ambapo mgombea wa ACT Wazalendo, Ali Abdallah alipata kura 1,026. 

Mbali na majimbo hayo, pia Chama Cha Mapinduzi kimeendelea kuwatesa wapinzani wake ambapo jimbo la Namtumbo, Edwin Ngonyani wa CCM alipata ushindi wa kishindo baada ya kupata kura 41,954 wakati mgombea wa CUF Bonifasia Mapunda alipata kura  17,000  huku mgombea wa CHADEMA, Henry Njovu akiambulia kura 7000.

Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi huo, majimbo mengine ambayo yamechukuliwa na wagombea wa Chama Cha Mapinduzi ni jimbo la Songea mjini ambako hali haikuwa shwari kwa  mgombea wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, Joseph Fuime baada ya kushindwa kufurukuta mbele ya mgombea wa CCM, Leonidas Gama ambaye aliibuka mshindi baada ya kupata kura 40,886 dhidi ya kura 37,200 alizopata mgombea huyo wa CHADEMA.

Jimbo la Peramiho, Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri mkuu sera, uratibu na bunge Jenista Mhagama alitetea nafasi yake kwa kupata kura 32,057  na kuwashinda wagombea wawili wa CHADEMA na ACT Wazalendo ambao walishindwa vibaya katika mchakato huo.

Wakati hayo yakiendelea wakili maarufu hapa nchini, Edson Mbogoro wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo naye aliangukia pua baada ya  kushindwa vibaya katika harakati zake za kutaka kuingia mjengoni (bungeni) na kujikuta akipata kura 5,649 huku mgombea wa Chama Cha Mapinduzi, Joseph Mhagama akishinda kwa kura 12,736.

Kwa mujibu wa duru za kisiasa, hii ni mara ya nne kwa  Edson Mbogoro kugombea ubunge katika majimbo mawili tofauti yaliyopo mjini hapa, ambapo mara  ya kwanza mwaka 2000 aligombea katika jimbo la Songea mjini na kushindwa huku marehemu, Dokta Lawrence Gama akishinda kwa kishindo na mwaka 2005 hadi uchaguzi wa 2010 alishindwa tena na Mbunge aliyemaliza muda wake, Dokta Emmanuel Nchimbi akimshinda kwa kura nyingi.

Pia katika wilaya ya Mbinga yenye majimbo mawili ya uchaguzi, Mbinga mjini na vijijini mgombea wa Chama cha Mapinduzi jimbo la Mbinga mjini  Sixtus Mapunda aliibuka mshindi  kwa kura 28,364 dhidi ya mgombea wa NCCR Mageuzi Mario Millinga  aliyepata kura 13,102.

Katika jimbo la Mbinga vijijini msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Venance Mwamengo alimtangaza Martin Msuha wa CCM kuwa mbunge mteule wa jimbo hilo baada ya kupata kura  59,269 akifuatiwa na mgombea wa CHADEMA Benjamini Akitanda aliyepata kura 11,285.

Kadhalika kwa jimbo la Nyasa msimamizi wa uchaguzi, Jabir Shekimweri alimtangaza Mhandisi  Stella Manyanya wa CCM kuwa mshindi baada ya kupata kura 31,548 huku mgombea wa CHADEMA, Ngwata Saulo aliyepata kura 12,653.

Sambamba na hali hiyo, mkoa wa Ruvuma pia umeandikahistoria mpya ya kisiasa kufuatia kuingia kwenye baraza la madiwani wagombea wawili wa Chama cha Mapinduzi, kata ya Misufini Ismail Fakir (26) na mgombea katika kata ya mjini Shaibu Kitete (24) kuwa madiwani wenye umri mdogo kuliko madiwani wengine waliowahi kushika nafasi hizo, katika halmashauri za mkoa huo.

No comments: