Na Kassian
Nyandindi,
Songea.
WATU watano akiwemo na mtoto mdogo mwenye umri wa mwaka
mmoja, ambao ni wakazi wa kijiji cha Mapipili wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma
wamenusurika kupoteza maisha, baada ya kunywa kinywaji ambacho kinasadikiwa
kuwa na sumu.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Mihayo Msikhela
alisema kuwa watu hao walikunywa kinywaji aina ya togwa wakati walipokuwa
shambani wanalima.
Msikhela alifafanua kuwa tukio hilo, lilitokea Novemba 20
mwaka huu majira ya mchana baada ya kunywa kinywaji hicho walianza kujisikia
vibaya, ambapo walikuwa wanaharisha na kutapika.
“Walipoanza kuharisha na kutapika, walichukua jukumu la
kupeleka taarifa kwa mtendaji wa kijiji cha Mapipili aitwaye Neema Mponda,
ndipo Polisi tulipopata taarifa hizi tulikwenda huko kuwachukua na kuwafikisha Hospitali
ya wilaya ya Mbinga, kwa ajili ya matibabu zaidi”, alisema Msikhela.
Kwa upande wake akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi
wetu, mganga mfawidhi wa Hospitali hiyo Robert Elisha alithibitisha juu ya
tukio hilo na kuwapokea huku akiwataja kwa majina kuwa ni Edda Komba (25),
Adelina Nchimbi (23), Paulina Komba (21), Stamily Mapunda (21) na mtoto mmoja
mdogo Stella Komba mwenye umri wa mwaka mmoja.
Elisha alibainisha kuwa hali zao zinaendelea vizuri na kwamba
kinywaji walichokunywa aina ya togwa kiliwasababishia maumivu ya tumbo na
wakaanza kuharisha na kutapika.
“Tumechukua hatua za haraka kuwapatia matibabu, lakini hatuja
ona katika kile kinywaji kama kulikuwa na sumu na watu hawa bado wapo chini ya
uangalizi wa madaktari wanaendelea vizuri na afya zao zitakapoimarika,
wataruhusiwa kwenda makwao”, alisema.
No comments:
Post a Comment