Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imefanikiwa kuvuka
lengo katika upimaji wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kwa asilimia 19.23 katika
kipindi cha mwaka huu kwa ufaulu wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na masomo
ya kidato cha kwanza, mwaka wa masomo 2015/2016.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu. |
Hayo yamebainishwa na Ofisa elimu ya msingi wa wilaya ya
Mbinga, Samweli Komba kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo, Venance
Mwamengo ambapo ufaulu huo umeongezeka kutoka aslimia 57 ya mwaka 2014
hadi kufikia asilimia 76 mwaka huu.
Hali hiyo imetokana na kuwepo kwa mikakati thabiti iliyowekwa
na idara ya elimu ya msingi wilayani humo, kuhakikisha kwamba hakuna
mwanafunzi asiyejua kusoma, kuandika na kuhesabu kuanzia darasa la kwanza
hadi la darasa la saba jambo ambalo mpaka sasa limefanikiwa katika utekelezaji
wake.
Komba alisema mwaka 2014, shule zilizofanya mtihani wa
Taifa kumaliza darasa la saba zilikuwa 217 ambapo jumla ya wanafunzi 7,561
walifanya mtihani huo na wanafunzi 4,303 sawa na asilimia 56.92
walibahatika kuchaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari.
Kutokana na matokeo hayo, idara ya elimu kwa
kushirikiana na Mkuu wa wilaya hiyo, Senyi Ngaga na wadu wengine iliendelea
kuboresha kwa kuwa na mitihani minne ya majaribio ambapo ufaulu wake,
ulikuwa mtihani wa kwanza asilimia 33, wa pili asilimia 72, wa tatu 74 na wanne
asilimia 80 hali iliyosababisha kuwa na picha ya matokeo mazuri kwa mtihani
huo wa darasa la saba kitaifa kuwa mzuri.
Kwa mujibu wa Komba alifafanua kuwa, matokeo ya mwaka huu 2015 Halmashauri imekuwa ya kwanza kimkoa, ambapo wanafunzi walioandikishwa walikuwa 6,003 waliofanya mtihani walikuwa 5,887 na wasiofanya ni wanafunzi 114 ambapo kati ya
idadi hiyo, waliofanya mtihani zaidi ya watoto 5,000 wamechaguliwa kujiunga na
kidato cha kwanza katika shule za sekondari.
Hata hivyo, licha ya mafaniko makubwa waliyoyapata bado
wanakabiliwa na changamoto kubwa, ya uwepo wa wanafunzi wanaoshindwa kufanya
mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kila mwaka, kutokana na sababu mbalimbali.
Komba ametaja changamoto zilizopo ikiwemo ya utoro, ugonjwa,
vifo, uhaba wa miundombinu kama vile nyumba za walimu, vyumba vya madarasa na
kwamba jamii inahamasishwa kuchangia ili kupata miundombinu inayokidhi idadi ya
watoto shuleni, hata hivyo mwitikio umekuwa mdogo kwa jamii kushiriki katika
shughuli za kujitolea.
Alisema baadhi ya wazazi wilayani humo, wamekuwa wakiwatumia
watoto kwenye shughuli za kiuchumi, kama vile mashambani kwa lengo la kujiongezea
kipato, hata hivyo wanaendelea kutoa elimu na kukemea juu ya madhara ya
kuwatumikisha watoto wenye umri wa kwenda shule kufanya kazi za nyumbani.
No comments:
Post a Comment