Na Bashir Yakub,
KUONGEZEKA kwa makampuni na taasisi
mbalimbali kumeleta wingi wa ajira
maeneo mbambali ya nchi. Mbali na kuongezeka
kwa ajira kumekuwepo na tatizo kubwa la
waajiriwa kutojua haki zao mbalimbali wanapokuwa
katika maeneo yao ya kazi.
Niseme jambo moja tu kuwa
hakuna suala la msingi kama muajiriwa kujua
haki zake. Hii ni kwasababu kupitia kujua
haki zake ndipo anapoweza kupata ujira stahiki,
posho stahiki, masurufu stahiki, mafao stahiki, malipo stahiki
ya kuachishwa kazi ikiwa ni pamoja na
ujumla wa kufanya kazi kwa misingi ya
kazi.
Ni muhimu kila mfanyakazi kupitia
haki zake mara kwa mara ili kujua
nini anapata na nini hapati. Uwe kazini au
umeachishwa bado ipo nafasi ya kudai
haki hizi ili upate kilicho chako.
Ukitegemea mwajiri ndio akwambie
haki zako, utakuwa unajidanganya kwasababu
yawezekana kabisa faida kubwa ya mwajiri
ipo kati ya wewe kutokujua haki zako. Ni
hasara kubwa kufanya kazi bila kujua haki
zako, kutokana na hilo leo nitaeleza
baadhi ya haki za mfanyakazi.
1. HAKI YA KUJUA SEHEMU YA
KUFANYIA KAZI.
Isiwe uliambiwa eneo la kazi
ni Dar es salaam, halafu ujikute kila
siku una safari za mikoani halafu
uambiwe eti hiyo ndiyo kazi yenyewe,
hapana. Lazima eneo la kufanyia kazi
lijulikane kwa mfanyakazi. Ijulikane kuwa
umeajiriwa na eneo lako la kazi ni
Dar es salam au Mwanza au Kagera.
Hii ina maana kubwa kwakuwa
mfanyakazi asipojua eneo lake la kazi
hataweza kudai malipo yatokanayo na
kufanya kazi nje ya ofisi. Lakini iwapo
unajua eneo lako la kazi basi utakapokuwa
nje ya eneo la kazi yakupasa kudai
malipo ya ziada. Kwa hiyo hakikisha mwajiri
wako unakuainishia kwa uwazi kabisa eneo
lako la kazi na ulijue. Nje ya hilo eneo ni
malipo mengine ambayo ni nje ya
mshahara wa kawaida.
2. HAKI YA KUJUA
MAHALI/SEHEMU MWAJIRI ALIPOKUTOA.
Waweza kuwa unakaa Mwanza
lakini mwajiri amekuita kufanya kazi Dar es
salaam. Au makazi yako ni Arusha lakini
kazi iko Mbeya. Mazingira kama haya yanazaa
haki ya msingi unapokuwa umeajiriwa.
Umuhimu wake ni kuwa wakati
wa kustaafu au kumaliza mkataba au ikitokea
umeachishwa kazi, basi ni wajibu wa
mwajiri kuhakikisha anakusafirisha kutoka
eneo la kazi mpaka alipokutoa. Anatakiwa
kukusafirisha kwa kutoa usafiri au kutoa gharama
za usafiri ukasafiri mwenyewe. Hautoweza kupata
haki hii iwapo hujui kitu kama hiki.
3. HAKI YA KUJUA AINA YA
KAZI UNAYOTAKIWA KUFANYA.
Lazima kazi unayotakiwa kufanya
ijulikane vyema. Isiwe unafanya kila kazi
inayokuja mbele yako. Mchanganuo wa kazi uwe
wazi. Kama ni sekretari ijulikane
kazi ni zipi za kufanya.
Kama ni meneja ijulikane kazi
ni zipi na kwa mchanganuo wenye
kueleweka kabisa. Hii husaidia kutofanya kazi
ambazo si zako au kufanya kazi nje
ya makubaliano. Kwa kujua haki hii kazi
yoyote utakayopewa iliyo nje ya
mchanganuo wa kazi zako, utapatana upya na
malipo yake yatatakiwa kuwa nje ya
mshahara.
4. HAKI YA KUJUA MCHANGANUO WA
MSHAHARA.
Mshahara ni jambo moja lakini
mchanganuo wa mshahara huo ni kitu kingine.
Mwajiri anaweza kukwambia mshahara ni
laki saba. Swali ni je laki hiyo
saba inagawika vipi.
Ili uendane vizuri na haki
hii mara nyingi usiiangalie ile laki
saba isipokuwa angalia mchanganuo wa laki
saba. Lazima mwajiri aoneshe kati ya hiyo
laki saba mshahara kamili ( basic salary)
ni upi, kodi itakuwa kiasi gani,
posho ya usafiri itakuwa kiasi gani, posho
ya chakula itakuwa kiasi gani, posho ya
pango la nyumba ya mfanyakazi itakuwa
kiasi gani, fedha za mfuko wa hifadhi
ya jamii kiasi gani na makato mengine
yote ambayo hutokana na makubaliano kati
ya mwajiri na mwajiriwa yajulikane
vyema.
Hii husaidia hata kudai malimbikizo
kwa usahihi baada ya kazi kuisha.
Huwezi kupata stahiki zako kwa kiwango
unachotakiwa kulipwa hasa baada ya kazi
kuisha kama huyajui haya.
5. HAKI YA KUJUA AINA YA
MKATABA WA KAZI.
Wapo watu ambao wako makazini
na hela wanapata na maisha yanakwenda
lakini hawajui wanafanya kazi kwa mkataba
wa aina gani. Ni hatari kutojua aina
yako ya mkataba kwakuwa utalazimika kukosa
baadhi ya haki zinazotokana na mkataba
wako yakiwemo malipo na posho nyinginezo.
Lazima ujue kama mkataba wako
ni wa muda au wa kudumu. Mkataba
wa muda unao masurufu yake na wa
kudumu unao masurufu yake. Usipolijua hilo
utayakosa hayo masurufu. Mkataba wa muda wa
ajira ni ule ambao ni wa kipindi fulani
kwa mfano mwaka mmoja lakini waweza
kuongeza au miaka miwili n.k. Kwa hiyo ni
vyema upitie mkataba wako wa ajira ili ujue
ni wa aina ipi.
6. HAKI YA KUJUA KAMA KUNA
KIPINDI CHA MPITO.
Kipindi cha mpito hujulikana kama
probation period. Hiki ni kipindi ambacho
unakuwa umeajiriwa lakini ukiwa chini ya
uangalizi maalum wa kupima ufanisi wako
katika kazi.
Ni muhimu kuwekwa wazi kipindi
hiki kitaanza lini na kuisha lini na
ni haki zipi ulizonazo ndani ya kipindi
hicho. Nasema hivyo kwakuwa wapo watu ambao wamewekwa
katika kipindi hiki kwa miaka mingi tu
huku wakikosa stahiki kamili za ajira na
pia wakikosa hata stahiki za hicho
kipindi.
Hii si sawa na hulenga
kumminya mfanyakazi na kumfaidisha mwajiri.
Hivyo ni muhimu uambiwe kipindi hiki
kinaanza lini na kinaisha lini na una
haki gani ndani ya kipindi hicho.
MWANDISHI WA MAKALA
HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI
LA HABARI LEO KILA JUMANNE, GAZETI
JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI
NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241
bashiryakub@ymail.com
(Kwa hisani ya sheriayakub.blogspot.com)
No comments:
Post a Comment