Wednesday, November 25, 2015

WATAKIWA KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA MALARIA



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

JAMII wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, imetakiwa kuhakikisha inachukua tahadhari mapema juu ya ugonjwa hatari wa malaria ambao unatajwa kuongoza kuwaua watu wengi, hapa nchini.

Rai hiyo imetolewa na Kaimu mganga mkuu wa wilaya hiyo, Adela Mlingi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari  ofisini kwake ambao walitembelea  Hospitali ya wilaya  ya Mbinga kujionea mkakati wa serikali katika kudhibiti magonjwa hatari ikiwemo malaria, kipindupindu, maambukizi mapya ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), vifo vya akina mama wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano. 

Mlingi alisema kulingana na ukubwa wa tatizo la ugonjwa huo, jamii inapaswa kutambua kwamba ni wajibu wao kuchukua  tahadhari  ya magonjwa hayo mapema, badala ya kuiacha serikali peke yake ambayo kwa upande wake imejitahidi kwa kiasi kikubwa kupambana nayo kwa kutafuta dawa na vifaa tiba. 


Alisema ugonjwa wa malaria kwa kiasi kikubwa unaambukizwa na mbu, hivyo wananchi wanahimizwa kutumia chandarua chenye dawa kila wanapokwenda kulala, ili kujikinga na ugonjwa huo hatari ambao unasababisha kupungua kwa nguvu kazi ya taifa. 

“Watu wengi wanauchukulia ugonjwa huu wa malaria, kama ugonjwa wa kawaida huku wakisahau kwamba ndiyo unaongoza kwa vifo vingi kuliko hata ukimwi”, alisema Mlingi.

Kutokana na hali hiyo, amewataka wananchi katika wilaya ya Mbinga pindi wanapohisi homa kwenda haraka hospitali kwa ajili ya kupata vipimo, ushauri na matibabu badala ya kuamua kumeza dawa bila ya kujua homa yake, jambo ambalo linaweza kuleta madhara makubwa kwao kiafya.

Mlingi alifafanua kuwa hivi sasa wananchi wanapaswa kubadilika kitabia na kuzingatia taarifa mbalimbali zinazotolewa na wataalamu wa afya, hatua ambayo itasaidia  kuacha  tabia ya kunywa dawa za malaria na magonjwa mengine bila kupata vipimo sahihi.

No comments: