Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kwamba, upatikanaji hafifu wa vifaa tiba,
vitenganishi na upungufu wa watumishi wenye taaluma katika kitengo cha huduma
za afya ya uzazi na mtoto wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, kunaathiri utoaji wa
huduma husika kwa wagonjwa.
Vilevile uhaba na ubovu wa magari, katika vituo vya afya kwa
ajili ya kubebea wagonjwa ili kuwezesha rufaa ya wazazi na watoto, nalo limekuwa
tatizo sugu na changamoto kubwa inayoikabili sekta hiyo ya afya wilayani humo.
Hayo yamebainishwa katika taarifa ya utekelezaji ya huduma za
afya ya uzazi na mtoto wilayani Mbinga, kwa mwaka 2015 ambapo wilaya ina jumla
ya vituo 63 vya huduma.
Mary Ngonyani ambaye ni Mratibu wa huduma hizo, katika
taarifa yake alisema pia mwitikio wa akina mama kuwahi kliniki bado upo chini
na hilo linatokana na hisia binafsi za akina mama, licha ya kuendelea kuhamasisha na elimu
kutolewa mara kwa mara.
Kadhalika alisema kuwa akina mama wajawazito 1,982
walijitokeza na kupima Kaswende, ambapo
kati yao 64 waligundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo sawa na asilimia
3.2 ya waliopima.
“Wajawazito 5,852 walipimwa virusi vya ukimwi sawa na
asilimia 77.7 ya ufikiwaji wa mahudhurio manne, kati yao 146 sawa na asilimia 2.4
waligundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo”, alisema.
Ngonyani alibainisha kuwa mimba zenye umri mdogo, zimekuwa
zikiongoza wilayani humo kwa asilimia 50.3 na akina mama wenye vidokezo vya
hatari waligundulika kuwa navyo, ikiwa ni sawa na asilimia 49.9 ya
waliohudhuria vipimo vya kitabibu.
Huduma ya uzazi wa mpango inatolewa kwenye vituo 54 vya
huduma, ikiwa ni asilimia 78.2 ambapo uhamasishaji na utoaji wa huduma za uzazi
unafanyika kupitia wataalamu waliopo katika vituo hivyo na hospitali ya wilaya,
na kwamba katika kipindi cha mwezi Januari hadi Juni mwaka huu huduma hiyo
ilitolewa kwa akina mama 17,189 sawa na asilimia 56.2 ya walengwa.
Hata hivyo Mratibu huyo alieleza kuwa huduma za afya ya mtoto
zimekuwa zikitolewa, jumla ya watoto 5,966 wamepata huduma ya chanjo katika
kipindi hicho ambapo watoto 184 kati ya hao walizaliwa na akina mama wenye
virusi vya ukimwi, watoto 179 walichukuliwa damu kwa uchunguzi zaidi ya ugonjwa
huo na kwamba kati yao watoto sita
waligundulika kuwa nao ambapo mmoja alifariki dunia na waliobakia wanaendelea
kupatiwa matibabu katika kitengo cha ushauri nasaha (CTC).
No comments:
Post a Comment