Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
CHAMA Cha Walemavu Tanzania (CHAWATA) tawi la Mbinga mkoa wa
Ruvuma kimesema, ifikapo siku ya maadhimisho ya watu wenye ulemavu Desemba 3
mwaka huu wilaya ya Mbinga itafanya maadhimisho hayo, kwa kuwapatia walemavu wake
mahitaji mbalimbali na sio kufanya sherehe kama ilivyozoeleka katika miaka
iliyopita.
Mwenyekiti wa chama hicho wilayani humo, Martin Mbawala
alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu juu ya mikakati ya
kuwasaidia walemavu na kuwainua kutoka katika umaskini, ambao umekithiri
miongoni mwao.
Alisema kuwa kufanya hivyo ni kuunga mkono agizo lililotolewa
na Rais John Magufuli kwamba, hakuna sababu ya msingi ya watu kufanya sherehe
ya kupika vyakula na kulipana posho kwa maadhimisho ya sherehe mbalimbali, bali
fedha husika zikatumike katika shughuli za kimaendeleo.
“Ni vyema Chawata hapa Mbinga tukaweka maadhimisho yetu kwa
mtindo huu, itakuwa sio busara kuliacha kundi hili tete litaabike kutafuta
mahitaji muhimu kama vile fimbo nyeupe za kutembelea kwa watu wasioona, halafu
tunatumia fedha nyingi kupika wali, kula nyama na kununua vinywaji ni vyema
sasa fedha hizi zielekezwe kununua mahitaji maalum ya watu hawa”, alisema
Mbawala.
Mbawala aliongeza kuwa chama hicho cha walemavu wilayani humo,
katika kufanikisha hilo kimejiwekea pia mipango yake madhubuti ya kutafuta
wahisani mbalimbali ambao wataweza kusaidia watu wenye ulemavu wilayani humo,
kwa kuwapatia mahitaji maalum yatakayo wawezesha kusonga mbele katika maisha
yao ya kila siku.
Hata hivyo alifafanua kuwa walemavu wengi wilayani Mbinga, wanahitaji
kusaidiwa baiskeli za kutembelea (Wheel chair), fimbo nyeupe, magongo, miwani
na mafuta ya kupaka watu wenye matatizo ya ngozi (Albino).
No comments:
Post a Comment