Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. |
Na Muhidin Amri,
Songea.
BAADHI ya wananchi katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,
wamefurahishwa na uteuzi wa Mbuge wa Jimbo la Ruangwa mkoani Lindi, Kassim
Majaliwa kuwa Waziri mkuu wa Tanzania, katika serikali hii ya awamu ya tano.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mjini hapa, walisema kuwa Majaliwa
ndiye mtu sahihi anayefaa kushika wadhifa huo kutokana na utendaji wa
kazi zake alipokuwa Naibu waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) anayeshughulikia elimu.
Mmoja wa wakazi hao, Thomas Komba alisema ni mtu ambaye
ataendana na kasi ya Rais Magufuli lakini pia wakati wote amekuwa kiongozi
mwadilifu na mchakapakazi hodari, ambaye hana makundi.
Dokta Magufuli katika utendaji wake wa kazi, alioonesha
tangu alipoingia Ikulu kwa mara ya kwanza siku chache zilizopita alidhihirisha
wazi kwamba serikali yake inahitaji watu makini ambao sio wazembe, katika kuamua
mambo mbalimbali ya maendeleo ili kuweza kukuza uchumi wa nchi.
Naye Mariam Yusuf, mkazi wa mtaa wa Misufini kata ya Misufini
mjini Songea alisema kuteuliwa kwa Majaliwa kuwa Waziri mkuu ni ishara tosha
kwamba serikali ya awamu ya tano, ni watu wa ‘hapa kazi tu’ ambao wanahitaji
kuwatumikia Watanzania ipasavyo.
"Kwa kweli mimi nikiwa mfuasi wa Chama Cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) sasa nina imani na serikali hii ya Dokta Magufuli, hata
huyu aliyetangazwa kushika nafasi ya Waziri mkuu ni mtu sahihi anayetambua
majukumu yake ya kila siku, tutamuunga mkono katika utekelezaji wa maendeleo ya
wananchi”, alisema Mariam.
Nao baadhi ya waandishi wa habari wa mkoa wa Ruvuma, hawakubaki
nyuma kuonesha imani yao kwa Majaliwa ambapo Julius Konala licha ya
kumpongeza Waziri huyo amewataka Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama
vyao kumuunga mkono, katika utumishi wake wote ili kumsaidia Rais Magufuli
katika mapambano dhidi ya vitendo viovu, vilivyokuwa vikifanywa na baadhi ya
watumishi wa umma hapa nchini.
Alisema, Dokta Magufuli na Majaliwa ni viongozi makini ambao
wataweza kuivusha nchi yetu katika mapambano dhidi ya rushwa, dhuluma na wizi
ambavyo vilisababisha hata wananchi kukata tamaa na kushindwa kuunga mkono mambo
ya kimaendeleo.
Naye Cresensia Kapinga mbali na kukunwa na uteuzi huo,
amewaomba viongozi wengine watakaoteuliwa katika serikali ya awamu ya tano kuwa
watu wanaowajibika katika majukumju yao ya kila siku, busara na uaminifu.
Aliongeza kwamba, kwa imani aliyonayo ni dhahiri kuwa viongozi hao wawili ndiyo watakaorudisha heshima ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwani baadhi ya wananchi walitofautiana kwa kile alichoeleza kuwepo kwa baadhi ya watu ndani ya serikali, kutokuwa na uwezo katika utendaji wa shughuli za kila siku.
No comments:
Post a Comment