Na Muhidin Amri,
Songea.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Songea mkoani Ruvuma,
kimeibuka kidedea baada ya mgombea wake wa udiwani katika Kata ya Mahanje jimbo
la Madaba wilayani humo, Stephano Mahundi kufanikiwa kushinda katika kiti hicho
baada ya kumshinda mgombea wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Hans
Mlelwa.
Uchaguzi huo ulishindwa kufanyika mwezi uliopita, baada ya kukosekana
kwa karatatsi za kupigia kura kwa nafasi ya udiwani, hata hivyo katika nafasi
ya ubunge na rais uchaguzi uliendelea kama uilivyopangwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC).
Akitangaza matokeo hayo msimamizi wa uchaguzi kata ya Mahanje,
Kanisius Lingowe alimtangaza mgombea huyo wa CCM kuwa mshindi baada ya
kufanikiwa kupata kura 946, dhidi ya mgombea wa CHADEMA Hans Mlelwa
aliyeambulia kura 487 ambaye hata hivyo, hakuwepo katika chumba cha kutangaza
matokeo hayo.
Lingowe alifafanua kuwa, katika kata hiyo jumla ya wananchi waliojiandikisha
walikuwa 12,325 waliojitokeza kupiga kura ni 1,449 huku kura halali zilikuwa 1,433
na kwamba zilizoharibika kulikuwa na kura 16.
Kwa mujibu wa msimamizi huyo wa uchaguzi, alisema sheria ya Tume
ya taifa ya uchaguzi inayo mamlaka ya kutangaza matokeo ya kura zilizopigwa na
kumtangaza mshindi, hata kama wagombea hawatakuwepo eneo husika na tume
itakachofanya ni kuwapa taarifa wagombea hao.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Mahundi ameahidi
kusimamia shughuli mbalimbali za maendeleo katika kata hiyo sambamba na
kuwatumikia kikamilifu wakazi wa Mahanje, ikiwemo namna ya kuboresha
huduma za kijamii kama vile afya, maji, elimu na miundombinu kwa baadhi ya
maeneo.
Mahundi alisema, jambo la kwanza atakalolipa kipaumbele ni
kuhakikisha wakazi wa kata hiyo wanakuwa na shughuli za kufanya ili kujipatia
kipato halali na kukomesha tabia ya kukaa vijiweni kwa muda mrefu, jambo
linalochangia umaskini licha ya ukweli kwamba, kuna rasilimali nyingi ambazo
bado hazijatumika kikamilifu.
Aidha, ameahidi kushirikiana na serikali, wataalamu wake
waliopo na wadau wengine wa maendeleo kuanzisha vikundi mbalimbali vya
ujasiriamali, kama vile wanawake na makundi ya vijana ili waweze kuondokana na
tatizo la ukosefu wa ajira ambao umekuwa kama wimbo kwa makundi hayo hapa
nchini.
Mbali na hilo, Mahundi alisema atatoa ushirikiano kwa
vyombo vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha kata hiyo na jimbo lote la Madaba,
kunakuwa na amani na utulivu ili kutoa nafasi kwa wananchi kufanya shughuli za
kiuchumi badala ya kutumia muda wao kutafuta suluhu ya migogoro, kitendo ambacho
kinaweza kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi.
Kutokana na hali hiyo, diwani huyo mteule amewataka wakazi wa
kata hiyo akiwemo aliyekuwa mshindani wake kisiasa kumpatia ushirikiano wa
kutosha katika majukumu yake mapya, ili aweze kutekeleza ahadi zote alizotoa
kwa wananchi badala ya kuendelea kununiana, kwani tayari uchaguzi umekwisha na kwamba
kuna maisha mbele ambayo wananchi wanahitaji maendeleo.
No comments:
Post a Comment