Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
WANANCHI wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, watanufaika na
mpango uliowekwa na Wakala wa misitu na nyuki wilayani humo, wa kuwagawia mbegu
za miti na kwenda kuotesha katika vitalu maalumu, ili baadaye iweze kupatikana
miche ya miti ambayo itapandwa katika maeneo mbalimbali ndani ya wilaya hiyo.
Vicent Mwafute. |
Mpango huo, umekuwa ukitekelezwa kupitia vikundi ambavyo
vimesajiliwa kisheria ambapo hupewa mbegu na kwenda kuzalisha miche ambayo
baadaye husambazwa kwa wananchi, kwa ajili ya kwenda kuipanda katika mashamba
yao.
Ofisa misitu wa wilaya hiyo, Vicent Mwafute alisema hayo
alipokuwa akihojiwa na waandishi wa habari juu ya suala la utunzaji wa
mazingira na misitu wilayani Mbinga.
Alisema kuwa tayari kilo 120 za mbegu ya miti rafiki ya maji,
zimenunuliwa na kupelekwa kwenye vikundi husika, ili waweze kuzalisha katika
vitalu na baadaye isambazwe kwa wananchi tayari kwa kupanda.
“Hivi sasa uelewa umekuwa mkubwa kwa wananchi hapa wilayani juu
ya umuhimu wa upandaji miti, mimi na wenzangu katika idara yetu tumekuwa
tukijitahidi kuwahamasisha na sasa jambo hili lina mwitikio mkubwa”, alisema
Mwafute.
Kadhalika aliongeza kuwa lengo la wilaya, katika kipindi hiki
cha mwaka 2015/2016 ni kuzalisha miche milioni 3 na kuifikisha kwa wananchi,
ili waweze kuipanda katika mashamba yao hasa
kipindi hiki cha kuelekea msimu wa mvua za masika.
Vilevile kwa upande wa udhibiti vitendo vya uchomaji moto,
katika misitu iliyopo wilayani humo, Mwafute alisema ni changamoto kubwa ambayo
wamekuwa wakikabiliana nayo hasa kipindi cha kiangazi kutokana na baadhi ya
watu kwa makusudi, wamekuwa wakiichoma moto pasipokuwa na sababu yoyote ile ya
msingi.
Alifafanua kuwa kufuatia hali hiyo, wananchi wanaendelea
kuelimishwa waweze kuachana na tabia hiyo na kwamba Halmashauri ya wilaya ya
Mbinga imekuwa ikiwasaka wahusika wa vitendo hivyo na kuwachukulia hatua za
kisheria, ili iwe fundisho kwa wengine kwa lengo la kudhibiti visiweze
kuendelea.
Zao la misitu katika Halmashauri hiyo ni
la tatu katika kuwaingizia mapato hivyo kutokana na umuhimu huo wataalamu wa
idara ya misitu na wadau mbalimbali, wamekuwa bega kwa bega kuhakikisha kwamba
misitu inaendelezwa ipasavyo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.
No comments:
Post a Comment