Na Muhidin Amri,
Namtumbo.
MKUU wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Chande Nalicho amekemea
tabia ya baadhi ya watu wasiojulikana kuhujumu miradi ya barabara
ikiwemo kung’oa alama za barabarani, ambazo husaidia watumiaji kutambua vizuri wanapokuwa
barabarani na kuepusha ajali zisizokuwa za lazima.
Nalicho ametoa kauli hiyo kufuatia kuwepo kwa baadhi ya watu,
kuanza kuharibu alama zilizowekwa barabarani katika barabara mpya ya Namtumbo
hadi Songea ambayo ujenzi wake, umekamilika na kuanza kutumika.
Alisema kuwa licha ya uharibifu huo unaofanywa na watu hao, wamekuwa
pia wakiiba baadhi ya vifaa kama vile mabomba na alama nyingine ambazo husaidia
watumiaji wake kutambua na kuwa waangalifu wanapokuwa barabarani, jambo ambalo husaidia
kupunguza kiwango cha ajali hasa kwa watembea kwa miguu.
Kadhalika alieleza kuwa ni vyema watanzania wakawa na tabia
ya kuthamini na kutunza miradi yao, ambayo serikali hutumia fedha nyingi
kuijenga kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi wake.
“Ninachowataka hapa wananchi watunze miradi hii ya maendeleo katika
wilaya yetu, serikali inatumia gharama kubwa kuijenga kwa manufaa yetu sisi wananchi
kwa kizazi cha sasa na kijacho”, alisema Nalicho.
No comments:
Post a Comment