Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli. |
Na Steven Augustino,
Tunduru.
WAFUGAJI jamii ya Kisukuma, wanaoendesha shughuli zao za
ufugaji wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma wamemuomba Rais wa awamu ya tano,
Dokta John Magufuli, kuwasaidia kudhibiti migogoro ya wafugaji na
wakulima ambayo inaendelea wilayani humo.
Hayo yalisemwa na wafugaji hao, katika sherehe ya kumpongeza
Dokta Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zilizofanyika
kwenye kambi yao ya wafugaji iliyopo kijiji cha Masonya wilayani hapa.
Kiongozi wa wafugaji hao Lugwasha Mtegwambuli, alisema kuwa
kufumbiwa macho kwa migogoro hiyo ambayo imedumu kwa muda mrefu sasa, imekuwa
ikigharimu maisha yao na kuwafanya waishi kama wakimbizi.
“Tunampongeza Dokta Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa
Tanzania, tunaimani naye kubwa katika utendaji wake wa kazi ili wananchi aweze
kutufikisha katika maendeleo ya kweli”, alisema Mtegwambuli.
Aidha alimuomba Rais Magufuli, kuimarisha usalama kati ya
wananchi na wawekezaji tofauti na sasa ambapo baadhi yao wamekuwa wakikiuka
taratibu na kuleta madhara kwa jamii, zinazowazunguka katika maeneo yao ya
wafugaji.
Mtegwambuli alisema kuwa wapo baadhi ya wawekezaji wamekuwa
wakijifanya miungu watu, wamekuwa wakitoa adhabu kali kwa wananchi wanaowazunguka
pindi inapotokea wameingia katika maeneo ya miradi yao.
Alifafanua kuwa wamekuwa wakipata madhara makubwa, ikiwemo
watu na mifugo yao huku wengine wakipoteza maisha kwa kupigwa risasi kwa madai
kwamba, wanaingia katika maeneo ya miradi ya hifadhi bila kibali maalum.
Kiongozi huyo wa wafugaji wilayani Tunduru alieleza kuwa, endapo
serikali haitaweka mikakati ya kudumu juu ya kumaliza tatizo hilo, uwezekano wa
kuondoka kwa manyanyaso dhidi ya jamii hizo hayatakoma badala yake
yatakuwa yakiendelea na kuathiri jamii.
Naye Thomas Matindi, ambaye ni mfugaji kijiji cha Kidodoma
wilayani humo pamoja na mambo mengine aliiomba serikali kuwatambua
wafugaji kwani wamekuwa kwa kiasi kikubwa wakichangia pato la Taifa, kupitia
mifugo yao.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Khalifa Makunganya alisema kuwa
katika kipindi chote wamekuwa wakiishi vizuri na wafugaji hao na kwamba,
wamekuwa wachangiaji wazuri katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Wafugaji hao ambao kwa sasa takribani wana ng'ombe 28,000
wilayani Tunduru, walianza kufanya shughuli hizo wilayani humo mwaka 2007 baada
ya serikali kuwaondoa katika bonde la Ihefu mkoani Mbeya, kwa lengo la
kuwapeleka katika mikoa ya Lindi na Mtwara ambapo walibakia hapa wilayani,
baada ya tamko la serikali la kuwataka wabakie katika maeneo hayo ili kuepusha
homa ya Bonde la ufa iliyozuka wakati wakiwa safarini kuelekea katika mikoa
hiyo.
No comments:
Post a Comment