Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
TANGU kifo cha Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius
Nyerere kilipotokea katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas mjini London nchini Uingereza,
hatuna haja ya kurudia ni kiasi gani Watanzania, Afrika na dunia kwa ujumla
wake, walivyoguswa na kifo hicho kila mmoja wao kwa nafasi yake, bali itoshe
kusema kwamba ulikuwa ni msiba wa dunia.
Licha ya machungu yaliyopatikana kutokana na kifo hicho,
Watanzania tunayo faraja kubwa kwa sababu mambo karibu yote, aliyoyapiga vita
Mwalimu Nyerere katika uhai wake ili kuleta haki na ukombozi kamili kwa
Watanzania, yameleta matunda yaliyotarajiwa.
Benedict Ngwenya. |
Mambo hayo ni ukoloni, ukoloni mamboleo na kila aina ya
ubaguzi, ikiwa ni pamoja na ubaguzi wa rangi, dini, ukabila na jinsia, rushwa
na maadui watatu wakubwa aliowatangaza baada ya kupata Uhuru mwaka 1961.
Maadui hao ni umasikini, ujinga na maradhi. Kwa kuyasoma
kwenye kumbukumbu mbalimbali na kuyasikia kwenye vyombo vya habari kwa maana ya
magazeti, redio, televisheni na kwenye mitandao ya kijamii hotuba zake zinaishi
kwa sababu zinagusa moja kwa moja, yanayotukabili Watanzania hivi sasa kama
vile anatushuhudia.
Hotuba hizo zinaishi, kiasi kwamba watu makini wanafarijika
ingawaje kwa wale ambao hotuba hizo zinawagusa kutokana na matendo yao machafu
ndani ya jamii, wanatamani wangevifungia vyombo vya habari husika, visiendelee
kutangaza taarifa hizo.
Alikuwa anayazungumza kuhusu ubaya wa rushwa na namna ya
kumpata kiongozi bora sifa zinazotakiwa awe nazo, bila kupotosha maneno na kwa
msisitizo unaostahili na lugha sanifu, kiasi kwamba ni kichaa peke yake anaweza
kujifanya hasikii au haelewi.
Katika hili sitachelea kuzungumzia juu ya sakata la kumpata
mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma,
ambapo wanambinga tunataka liendeshewe kwa amani na utulivu pasipo kujengeana
vitisho na dharau.
Benedict Ngwenya ambaye ni Katibu wa siasa na uenezi katika
mkoa huo, pia ni Diwani mteule wa kata ya Mpepai ambaye anasubiri kuapishwa
kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani hapa,………. naweza kusema
sasa anashangaza umma.
Ngwenya anadaiwa kuonekana wazi kuweka mikakati ya kupanga
safu za wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji huo, huku
akidaiwa kuwatisha baadhi ya wagombea wenzake kwamba, yeye ndiye mwenye uwezo
wa kuongoza nafasi hiyo na sio mwingine.
Naweza nikamtafsiri kwa kitendo hiki anachokifanya, ni sawa
na mtu mwenye uchu wa madaraka ambaye hataweza kuliongoza taifa hili changa la
wanambinga, kutokana na kuanza kuonesha hali hiyo mapema.
Mbinga inachangamoto tele za kimaendeleo zenye kuhitaji
kupiga hatua na kuongozwa na kiongozi shupavu, makini na mwenye kuweka kando
uroho wa madaraka.
Nikirejea kauli za hayati Mwalimu Nyerere enzi ya uhai wake,
alikuwa akikemea vitendo kama hivi na kuwaasa Watanzania kuepuka kuchagua
viongozi wa mtindo huu.
Mwalimu ni mtu ambaye alikuwa akiona mbali na kuchukizwa na
viongozi wa namna hii, natoa wito kwa ndugu zangu wanambinga ifike mahali kwa
mambo haya tunapaswa kuyapinga kwa nguvu zote, tugeuke nyuma na kufuata nyayo
za Mwalimu Nyerere.
Nasema, kitendo hiki kinachofanywa na Ngwenya ni dhahiri
utovu wa nidhamu ndani ya chama, viongozi wenye mamlaka ya uteuzi majina ya
wagombea wa nafasi hiyo ngazi ya mkoa, mnapaswa kuwa makini na kuzingatia
taratibu husika ili kusiweze kutokea mpasuko ambao hauna tija katika jamii.
Tukumbuke kwamba usiku wa kuamkia Juni 21 mwaka 2013,
kulitokea vurugu hapa Mbinga na kufikia hatua watu wasiojulikana walichoma moto
ofisi ya Chama wilaya kwa sababu tu ya dalili za mambo kama haya, tusingependa
kuona hali hii inajirudia tena.
Siku zote nimekuwa nikijiuliza, kibuli hiki anakipata wapi
kinachomfanya apite kutamba mitaani kana kwamba hii CCM ni ya kwake au huenda
kuna siri ndani yake imejificha, ndio maana anakuwa hivi?
Tunahitaji Mwenyekiti atakayekuwa na uchungu wa maendeleo na
kusimamia haki ndani ya baraza la Madiwani, atakayeweza kuwaletea wananchi
maendeleo na sio bora kiongozi ambaye muda mwingi anakaa kufikiria maslahi yake
binafsi.
Mamlaka za uteuzi wa majina ya wagombea zina kila sababu ya
kuzingatia taratibu husika bila kufanya upendeleo wa aina yoyote ile, rejesheni
majina ambayo ni chaguo la watu na sio kama Ngwenya anavyotamba mtaani na
kutishia wagombea wenzake kwamba, kwa nafasi aliyonayo atahakikisha majina
yatakayorudi ni yale ambayo ataweza kupambana nayo katika kinyang’anyiro hicho
cha kumtafuta Mwenyekiti ndani ya Halmashauri yetu.
Hii ni aibu kwa kiongozi kama huyu, tena ni Katibu wa siasa
na uenezi ndani ya mkoa wa Ruvuma, akifanya vitendo vya kukitia aibu chama hiki
tawala yatupasa kukemea hali hii kwa nguvu zote.
Aliyoyapigania Mwalimu Nyerere katika uhai wake, ndiyo
tunaweza kuthubutu kusema ni utamaduni wa Watanzania uliotuletea amani,
utulivu, upendo, mshikamano na umoja, sasa tusipozingatia haya sitakosea nikisema; “naliona
anguko la Benedict Ngwenya”.
No comments:
Post a Comment