Na Muhidin Amri,
Songea.
MKURUGENZI mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Madaba mkoani
Ruvuma, Robert Mageni amewataka Waandishi wa habari katika mkoa huo,
kusaidia kutangaza na kuandika fursa mbalimbali zilizopo katika halmashauri
hiyo hatua ambayo itasaidia kuvutia watu wengi, kwenda kuwekeza katika jimbo la
Madaba.
Mbali na wito huo, Mageni amewahimiza kuandika habari
nzuri zinazohamasisha wananchi kujikita katika shughuli za maendeleo hususani
kwa zile zinazofanywa na wakazi wa jimbo hilo, badala ya kuandika au kutangaza
habari za migogoro kwani zinaweza kuhatarisha kuharibu mahusiano yaliyopo
kati ya wananchi na serikali yao.
Mageni alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi
wetu ofisini kwake katika kijiji cha Madaba, mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi
mdogo wa udiwani kata ya Mahanje ambapo mgombea wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Stephano Mahundi, aliibuka mshindi dhidi ya mgombea wa Chama Cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA), Hans Mlelwa.
Mageni ameungana na wadau wengi katika mkoa wa Ruvuma, kupongeza
mchango mkubwa unaofanywa na waandishi wa habari hapa Ruvuma, kuandika habari
sahihi na zinazohamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za kimaendeleo.
Alisema kuwa, vyombo vya habari vikitumika vizuri vina
mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi hapa nchini, lakini iwapo vitatumika
vibaya vinaweza kuleta matatizo makubwa kama vile kuibuka kwa mifarakano kati
ya wananchi na serikali yao.
Pia alieleza kuwa amewataka wakazi wa jimbo hilo kuangalia
namna wanavyoweza kutumia fursa zilizopo, ili kujiletea maendeleo yao
badala ya kukaa na kusubiri kuona watu kutoka nje wakinufaika na rasilimali
hizo, jambo ambalo halipendezi.
Mageni amewahimiza pia, wakulima kuongeza uzalishaji wa mazao
ya chakula na biashara na kuahidi kuwa serikali itajitahidi kuwa karibu nao
katika suala la pembejeo za kilimo na kutoa ushauri wa kilimo cha kisasa, ili
kiwe na tija kwao kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.
No comments:
Post a Comment