Na Bashir Yakub,
TULIPOANDIKA namna bora na taratibu
maalum za kufuata unapotaka kununua ardhi,
tulisema pia taratibu za ununuzi wa ardhi
huwa zinatofautiana kutegemea na mazingira
ya kila ardhi. Tukasema unaponunua ardhi
kwa msimamizi wa mirathi, ni tofauti
na unaponunua kwa mmiliki mwenyewe.
Unaponunua ardhi ya familia ni
tofauti na unaponunua isiyo ya familia.
Vilevile unaponunua ardhi ya kijiji ni
tofauti na unaponunua ardhi isiyo ya kijiji. Taratibu
hutofautiana na hasa tofauti ipo katika
nyaraka ambazo zinatakiwa kuambatanishwa, ikiwa
kama ithibati ya ununuzi. Hata uandishi
wa mkataba wa manunuzi pia nao huwa na
tofauti katika hili.
1. ARDHI YA KIJIJI KWA UWEKEZAJI.
Wako watu wamekuwa wakinunua
ardhi hasa huko vijijini, lakini baadae
wamekuwa wakijikuta katika migogoro mikubwa
na wenyeji. Mwamko wa kununua maeneo kama
Bagamoyo, Kisarawe, huko Chanika Dondwe na maeneo
mengine umekuwa mkubwa sana. Hata hivyo
mwamko unavyoongezeka ndivyo na migogoro
inavyoongezeka. Kubwa katika migogoro hii ni
hatua ya wanunuzi kutokufuata utaratibu wa
ununuzi aidha kwa kujua, kutokujua au kupotoshwa.
Wakati mwingine ni uelewa mdogo
miongoni mwa wenyeji, lakini zaidi ni
hili la kutofuata utaratibu. Mara zote huwa
tunasema ni bora zaidi mgogoro unapotokea halafu
ukukute ulifuata taratibu wakati wa manunuzi.
Bila shaka hautakuwa na athari kubwa kwako,
lakini ni mbaya zaidi ukitokea halafu
ukukute kuna taratibu hukufuata kwa bahati mbaya
au bila kujua. Unakuwa katika hatari ya kupoteza.
Unapokwenda kununua ardhi ya kijiji
kwasababu yoyote ile hasa uwekezaji, upo
utaratibu maalum wa kufuata nitakaoeleza.
2. ARDHI YA KIJIJI NI NINI.
Ardhi ya kijiji ni ile
ardhi iliyopo katika mipaka ya kijiji
fulani, ilyoainishwa na mamlaka za wilaya
husika huku ikiwa na hati ya usajili
wa kijiji. Ardhi hii hulindwa kwa taratibu
za kimila za eneo husika, ikiwa ni
pamoja na sheria namba 4 ya 1999.
3. UTARATIBU WA KUNUNUA
ARDHI YA KIJIJI KISHERIA.
( 1 ) Maombi maalum huandaliwa na kuwasilishwa
kwa mtendaji wa kijiji ambaye
hupatikana katika kila kijiji.
( 2 ) Maombi huandaliwa katika fomu maalum
ambazo hupatikana katika kila ofisi za
kijiji. Si maombi ambayo huandaliwa kama
barua za kawaida za maombi.
( 3 ) Ikiwa mwombaji ni mtu mmoja
basi atasaini sehemu maalum na ikiwa
ni maombi kwa niaba ya famliia, basi
watu wawili kutoka ile familia watasaini
na ikiwa ni ardhi kwa ajili ya
kikundi pia wawakilishi wasiopungua wawili kutoka
kila kikundi watasaini kwa niaba ya
wengine.
( 4 ) Kama mwombaji ni chama cha ushirika
au kampuni, basi inatakiwa kuwepo wadhamini
wawili kwa ajili ya shirika au kampuni
hiyo. Wanaweza kuwa zaidi ya wawili lakini
wasipungue.
( 5 ) Kama anayeomba ardhi si mwenyeji wa
eneo husika, basi atatakiwa kuwa na
wadhamini wasiopungua watano ambao ni wenyeji
wa eneo hilo. Sharti ni kwamba kati ya
hao wadhamini wasiwepo ndugu wa mwombaji.
( 6 ) Mwombaji atatakiwa kuambatanisha katika maombi
yake tamko linaloonesha ardhi nyingine
anayoimiliki Tanzania nje na hiyo anayoomba.
( 7 ) Ikiwa ardhi inaombwa kwa ajili
ya makazi basi mwombaji atatakiwa
kuambatanisha tamko linaloonesha kuwa ataanza
ujenzi wa makazi hayo ndani ya miezi mitatu
tangu siku ya kuidhinishiwa ardhi.
( 8 ) Ikiwa mauzo ni ekari 50 au kuendelea ni
lazima yaidhinishwe na mkutano mkuu wa
kijiji.
( 9 ) Baada ya kukamilisha taratibu hizo
halmashauri ya kijiji itakaa vikao na
ndani ya siku tisini itatakiwa kutoa majibu.
Kamwe usikubali kuuziwa ardhi
ya kijiji na viongozi wa kijiji,
bila kufuata utaratibu huu. Hii hasa ni kwa
wawekezaji wanaochukua maeneo makubwa kwa
shughuli za kiuchumi.
MWANDISHI WA MAKALA
HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI
LA HABARI LEO KILA JUMANNE ,
GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI
NIPASHE KILA JUMATANO.
0784482959,
0714047241
bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment