Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
SERIKALI hapa nchini, imeombwa kujenga jengo jipya la kitengo
cha maabara katika Hospitali ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, kutokana na
jengo linalotumika sasa, halitoshelezi mahitaji husika.
Aidha kitengo hicho hivi sasa, kinakabiliwa na mapungufu ya
vitendea kazi ikiwemo vifaa tiba na dawa jambo ambalo husababisha wataalamu wa
maabara katika hospitali hiyo, wakati mwingine kushindwa kutekeleza majukumu
yao ipasavyo.
John Chihapula ambaye ni Mkuu wa kitengo cha maabara wilayani
Mbinga, alisema hayo alipokuwa akihojiwa na waandishi wa habari ambao
walitembelea hospitalini hapo, kwa lengo la kujionea changamoto mbalimbali
wanazokabiliana nazo.
“Jitihada za makusudi inapaswa zichukuliwe ili kuweza
kunusuru hali hii isiweze kuendelea, jengo letu la maabara limekuwa finyu
halitoshelezi mahitaji tunahitaji serikali ijenge jengo lingine kubwa, ambalo
litakidhi mahitaji ya utendaji wa kazi zetu za kila siku”, alisema Chihapula.
Chihapula alifafanua kuwa, hata wagonjwa wamekuwa wakipata
shida kutokana na jengo hilo kukosa sehemu ya kupumzikia, wakati wanaposubiri
majibu yao ya vipimo vya magonjwa badala yake hulazimika kusimama nje ya jengo
kwa muda mrefu.
Pamoja na mambo mengine, alieleza kuwa katika kukabiliana na
tatizo la upungufu wa vifaa tiba, serikali imekuwa ikifanya jitihada ya
kutafuta vifaa hivyo kutoka kwa wafadhili mbalimbali.
Alisema kufuatia kuwepo kwa jitihada hizo, hivi sasa
Hospitali ya wilaya ya Mbinga imepata mashine mpya ya kisasa, Gin Expert na
Darubini moja ambavyo hutumika kupimia magonjwa ya kifua kikuu na kwamba wakati
wowote itaanza kufanya kazi, baada ya taratibu husika kukamilika.
Mkuu huyo wa kitengo cha maabara wilayani humo, aliongeza
kuwa kutokana na hospitali kila siku hupokea wagonjwa wengi zaidi ya 200 wa matibabu
ya ndani na nje, kuna kila sababu ya kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma
bora kwa kuwa na vifaa tiba na dawa vinavyojitosheleza, ili kuondoa malalamiko
yasiyokuwa ya lazima miongoni mwa jamii.
No comments:
Post a Comment