Na Steven Augustino,
Songea.
WATU watatu wamefariki dunia, katika matukio mawili tofauti
yaliyotokea katika kijiji cha Madaba kata ya Mahanje wilaya ya Songea na kata
ya Makambi Manispaa ya Songea, hapa mkoani Ruvuma.
Akizungumzia matukio hayo Kamanda wa Polisi mkoani humo, Mihayo
Msikhela alisema kuwa matukio yote yalitokea November 16 mwaka huu na kwamba tukio
la kwanza lilitokea kijiji cha Madaba, kata ya Mahanje ambapo watoto wawili
walikutwa wakiwa wameungua moto na miili yao kuteketea kabisa.
Mihayo Msikhela, Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma. |
Kamanda huyo wa Polisi alisema kuwa tukio hilo la watoto
kuungua moto, lilisababishwa na mshumaa ambao waliwashiwa na mama yao mzazi ambaye
wakati tukio hilo linatokea alikuwa kwenye sherehe za kushangilia ushindi wa
Diwani wa kata Mahanje, Stephano Mahundi kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi mdogo uliofanyika November 16
mwaka huu.
Msikhela aliwajata marehemu hao kuwa ni, Happy Mgani (4) na
Chesco Mhagama (2) na kwamba mama huyo ambaye hakutaka kumtaja jina lake, yupo
chini ya ulinzi wa Polisi kwa mahojiano zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, mama huyo aliwafungia kwa nje
watoto hao na kwenda kwenye sherehe hizo ambapo hadi moto huo unawaka,
majira ya saa 8 za usiku alikuwa bado hajarejea nyumbani kwake.
Aidha Kamanda Msikhela alilitaja tukio jingine kuwa lilitokea
katika kata ya Makambi Manispaa ya Songea kwamba, mtu aliyefahamika kwa jina la
Ngaponda Khalifa (25) alifariki dunia baada ya kushambuliwa na wananchi wenye
hasira kali, baada ya kumchoma kisu mpenzi wake aliyefahamika kwa jina la Hawa
Swaleh (18).
Alisema katika tukio hilo Marehemu Khalifa alikwenda kwa
mwanamke huyo, kwa lengo la kumuomba radhi na kumtaka warudiane na kuishi kama
mume na mke na kwamba alichukua maamuzi ya kumchoma kisu, baada ya ombi lake kukataliwa.
Majeruhi Hawa ambaye ni mkazi wa kijiji cha Ligela, amelazwa
Hospitali ya mkoa wa Ruvuma (HOMSO) kwa matibabu zaidi na akaongeza kuwa Polisi
wamejipanga kufanya oparesheni ya kuwanasa waliohusika katika tukio hilo, ili
sheria iweze kuchukua mkondo wake.
No comments:
Post a Comment