Na Bashir Yakub,
KESI /shauri lolote iwe jinai
au madai kuishinda kwake mara nyingi
hutegemea mambo makuu mawili. Kwanza mashahidi, pili
ushahidi. Mashahidi siku zote ni watu. Hakuna
kitu kinaweza kuitwa mashahidi halafu
kisiwe binadamu. Hii ni tofauti na ushahidi.
Ushahidi si lazima wawe binadamu.
Vitu hasa vizibiti(exhibit) ndivyo huitwa ushahidi.
Nyaraka, mali, vifaa, na kila kitu ambacho
mtu anaweza kukitumia mahakamani kuthibitisha kile
anachokisema huitwa ushahidi. Yumkini yawezekana wakati
huohuo mmoja ukawa na vyote yaani
ushahidi pamoja na mashahidi hapo hapo. Hii hutegemea
namna mtu alivyojiandaa katika kuwasilisha
kesi yake.
1.SIFA ZA
SHAHIDI.
Si kila mtu ana sifa za
kuwa shahidi. Shahidi hutakiwa kuwa mtu mkweli,
muaminifu na muadilifu. Lakini pia sifa
kuu ya shahidi ni kuwa na akili
timamu. Mtu asiye na akili timamu
hawezi kuwa shahidi. Lakini pia mtu mwenye
sifa ya uongo hasa huko nyuma
kama aliwahi kutoa ushahidi wa uongo
mahakamani na ikathibitishwa kuwa alitoa
ushahidi wa uongo basi naye hupoteza
sifa ya kuwa shahidi.
Pia sifa nyingine kuu ya
shahidi ni muhimu awe ni yule
aliyeona, kuhisi kwa kutumia moja
kati ya viungo vyake, au kusikia .
Hii ina maana shahidi hutakiwa kuwa yule
anayelijua tukio kwa kulishuhudia na si
vinginevyo.
2. IDADI
YA MASHAHIDI INAYORUHUSIWA.
Hakuna idadi ya mashahidi rasmi
inayoruhusiwa kisheria. Idadi yoyote ya mashahidi
inaruhusiwa. Suala la msingi hapa ni
kuwa kila shahidi katika mashahidi hao
unaowaleta awe na umuhimu katika kesi.
Usilete watu ambao hawahusiki na
kuisababishia usumbufu mahakama. Hii ni kwasababu
wingi wa mashahidi hauakisi ushindi katika kesi.
Hata shahidi mmoja tu kama ni wa muhimu
anaweza kukufanya ushinde kesi na kumshinda
mwenye mashahidi ishirini.
3. JE
ALIYEAMBIWA ANAWEZA KUWA SHAHIDI.
Ushahidi wa kuambiwa siku zote
huwa haukubaliki mahakamani. Inatakiwa yule aliyekuambia
ndiye aje mahakamani na aseme hicho alichokiona
na kukusimulia wewe. Aliyeona, kusikia au kuhisi
jambo ndiye aje mahakamani na sio
amwambie fulani halafu huyu fulani eti
ndo awe shahidi. Ni mazingira machache
ambapo ushahidi wa kuambiwa unaweza
kukubalika, kwa mfano iwapo aliyekwambia amekufa n.k.
4.
KUMLAZIMISHA SHAHIDI KUFIKA MAHAKAMANI.
Kifungu cha 26 sheria ya
mwenendo wa mashauri ya madai kinasema
kuwa mahakama inaweza kutoa wito(summons)
kwa mtu yeyote ambaye ni shahidi
kufika mahakamani kutoa ushahidi wake
au kutoa (release) nyaraka yoyote ambayo
iko mikononi mwake. Hapa kuna mambo mawili, kwanza
yeye mwenyewe kufika mahakamani kutoa ushahidi.
Na pili kutakiwa kutoa (release)
nyaraka aliyonayo.
Wakati mwingine huwa inatokea kuwa nyaraka
fulani ambayo ndio ushahidi wako
unaotegemea iko mikononi mwa mtu mwingine/taasisi/kampuni
nyingine ambayo una uadui nayo au
huna uadui lakini unajua kwasababu moja
au nyingine hawawezi kukupa hiyo nyaraka
ukiiomba. Basi ndio hapo jambo
hilo utatakiwa kulisema mahakamani ili
utolewe wito wa kuwataka hao wahusika
kuleta nyaraka hiyo mahakamani kwa ajili
ya ushahidi.
5. HATUA
KWA KUKATAA KUTOA USHAHIDI.
Kifungu cha 27 sheria ya
mwenendo wa mashauri ya madai
kinasema kuwa iwapo mtu ameitwa kutoa
ushahidi au kuwasilisha nyaraka fulani na
amekataa kufanya hivyo basi mahakama itatoa
waraka wa kukamatwa kwake au kukamata mali
yake na kuiuza au kumtoza faini. Hivyo ndivyo
ilivyo.
MWANDISHI WA MAKALA
HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI
LA HABARI LEO KILA JUMANNE ,
GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI
NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959,
0714047241
bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment