Na Steven Augustino,
Tunduru.
VIONGOZI waliopo katika vijiji na kata wilayani Tunduru mkoa
wa Ruvuma, wameaswa kujenga ushirikiano kwenye vikao vyao vya maamuzi
mbalimbali ya kimaendeleo, ili waweze kuisaidia wilaya hiyo kufikia malengo na
utekelezaji wa ahadi zilizoahidiwa na viongozi wao, wakati wa kampeni za
uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ambao umefanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Hayo yalisemwa na Madiwani wateule kupitia tiketi ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao wamepewa ridhaa ya kuingia katika baraza la
madiwani la halmashauri ya wilaya hiyo, wakati walipokuwa wakitoa shukrani zao
kwa kuchaguliwa katika sherehe zilizofanyika kata ya Matemanga wilayani humo.
Diwani mteule kutoka kata ya Marumba, Msenga Said Msenga
alisema kuwa endapo wananchi hawatashiriki ipasavyo katika shughuli za
maendeleo, mafanikio yatachelewa kuwafikia katika maeneo yao hivyo wanapaswa
kujenga ushirikiano wa kutosha, ili kuweza kufikia malengo husika.
Alisema kuwa diwani kazi yake sio kubuni na kupeleka miradi katika
vikao peke yake, bali kazi yake ni kukaa na wananchi wake kupitia vikao vya
(WADC) na kujenga hoja za uibuaji wa miradi hiyo na kufanya ufuatiliaji ikiwemo
pia kusimamia miradi, ambayo imeibuliwa na kuipeleka ngazi ya juu kwa ajili ya
utekelezaji.
“Nawaomba viongozi
tuwashirikishe wananchi kwa kufanya nao vikao vya kupitisha maamuzi mbalimbali,
sio kukaa mezani na kutengeneza mambo ambayo wananchi hawajashirikishwa”,
alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tunduru, Hamis
Kaesa akatumia nafasi hiyo kuwaomba viongozi kuwashirikisha wananchi wakati wa
uibuaji wa miradi husika, na kuisimamia wakati wa kuipitisha katika vikao vya
maamuzi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Katibu mwenezi wa Chama Cha
Mapinduzi wilaya ya Tunduru, Aindi Daruweshi pamoja na kuwapongeza
wananchi kwa maamuzi hayo, alikiri kuwa chama chake kilipata wakati mgumu
walipokuwa kwenye kampeni za uchaguzi huo.
Daruweshi alisema kuwa ugumu huo, ulitokana na uwepo wa
wanachama mamluki ambao walikuwa sio waaminifu ndani ya chama.
Alitamba akisema kuwa katika uchaguzi huo, chama hicho
kimeibuka kidedea katika majimbo ya ubunge yaTunduru kusini na kaskazini, ambapo
kilipata madiwani 26 kati ya kata 39 zilizopo katika majimbo hayo.
No comments:
Post a Comment