Na Mwandishi wetu,
Madaba.
MKURUGENZI Mtendaji Halmashauri ya wilaya ya
Madaba mkoani Ruvuma, Robert Mageni amewataka watendaji wa vijiji, mitaa
na kata katika wilaya hiyo kushughulikia matatizo ya wananchi katika
maeneo yao ya kazi, na sio kuwaacha wakitaabika peke yao bila kupatiwa ufumbuzi
wa haraka.
Mageni alitoa rai hiyo alipokuwa akizungumza
na Madiwani wapya na Mbunge mteule wa Jimbo la Madaba, Joseph Mhagama wakati
wa hafla fupi ya kuwakabidhi vyeti vya utambulisho pamoja na kupeana mikakati
ya utekelezaji wa mipango mbalimbali yenye lengo la kuongeza kasi ya
maendeleo na ufanisi wa kuwatumikia wananchi, iliyofanyika mjini hapa.
Alisema jimbo hilo ni jipya, hivyo linahitaji
viongozi waliochaguliwa kuwa na mshikamano ili waweze kuboresha
huduma za kijamii, ambapo alitolea mfano kama vile ujenzi wa vyumba vya maabara
kwa shule za sekondari.
Mkurugenzi huyo alisema, watendaji wa serikali
hawapaswi kulalamika badala yake wao ndiyo wanatakiwa kuwa mfano wa kuigwa na
kuchukua hatua madhubuti, kumaliza kero za wananchi katika maeneo yao.
Aidha aliwataka watumishi hao kuwa na ushirikiano
na madiwani walioteuliwa kuongoza kata zilizopo ndani ya wilaya ya Madaba, kwa
kusimamia shughuli za maendeleo ya wananchi na kuwachukulia hatua za kisheria
watu wanaoharibu mazingira ikiwemo ukataji miti na uchomaji misitu hovyo,
ambao husababisha kuharibu na kupungua kwa vyanzo vya maji.
No comments:
Post a Comment