Na Bashir Yakub,
UNAPOMDAI mtu kupitia Mahakama
na hukumu ikatolewa kuwa ni kweli
unamdai na anastahili kukulipa, basi mtu
huyo hustahili kulipa. Lakini mara kadhaa
hutokea mtu kusema sina hela ya
kulipa au vinginevyo, ilimradi tu asilipe
deni.
Lakini pia madai hapa si lazima iwe hela tu, inayotokana na kukopeshana. Yapo pia madai ambayo hutokana na mtu kushinda kesi. Kwa mfano mwanamke alifungua kesi dhidi ya mme wake akitaka matunzo yake na ya mtoto/watoto.
Au shauri limekwisha na mtu
aliyeshindwa ametakiwa na Mahakama kulipa
gharama. Au malipo ya fidia na mengineyo
yote ambayo huamriwa na Mahakama kuwa
yalipwe. Haya yote unaweza kuyafanya
yalipwe kwa kukamata mshahara wa mhusika
kwa njia za kisheria.
Hatua hii imeelezwa katika amri ya 21 ya kanuni ya 47 sura ya 33 sheria ya mwenendo wa mashauri ya madai.
1.HATUA YA KUKAMATA MSHAHARA WA MTUMISHI.
Mahakama inapotoa hukumu ikimtaka mtu fulani kutekeleza jambo fulani au kulipa kiasi fulani kwa mtu fulani, amri hiyo hutakiwa kutekelezwa kwa hiari na si vinginevyo. Yule aliyeamrishwa hutakiwa kutekeleza kama alivyoagizwa na ndani ya muda alioelezwa.
Ikiwa atatekeleza bila kukosa basi
hatua hizi za kukamata mali zake
ikiwemo hii ya kukamatwa kwa mshahara
wake hazitachukuliwa. Hii ni kwakuwa atakuwa
ametekeleza kwa hiari. Hatua za kukamata
mali zake ikiwemo mshahara wake huchukuliwa
ikiwa kama njia ya kumlazimisha mtu
kutekeleza kile alichokataa kutekekeza kwa hiari
.
2. KUKAMATA MSHAHARA WA MTUMISHI WA SERIKALI.
Watumishi wa serikali huwa na taratibu za malipo ambazo zipo tofauti na taasisi binafsi. Lakini pia hata ndani ya serikali yenyewe idara na taasisi nazo huwa na taratibu tofauti katika malipo. Kwa mfano wapo watumishi ambao mishahara yao huanzia hazina na wapo ambao utaratibu wao wa mishahara hauanzii huko.
Hivyo basi ikiwa malipo ya
mtumishi huanzia hazina, basi mamlaka za
hazina zitapewa taarifa ya kimahakama itakayoeleza
kile alichofanya mtumishi, ikiwa ni pamoja
na ile amri ya kukamata mshahara wa
mtumishi kulipia deni kwa mujibu wa
hukumu na tuzo (decree). Wahasibu na
watoa malipo (cashier) watalazimika kufuata
vilevile kama ilivyoamriwa na mahakama.
3. KUKAMATA MSHAHARA WA MFANYAKAZI ASIYE WA SERIKALI.
Ikiwa mshahara unaotakiwa kukamatwa kufidia deni ni wa mfanyakazi asiye wa serikali, basi taarifa rasmi itatolewa kwa mwajiri wake kama ni kampuni, asasi ya kiraia au vinginevyo. Mwajiri atatoa taarifa hiyo kwa afisa anayehusika na malipo, ili kuanzia hapo mshahara wa mhusika utumike kulipia deni kwa mujibu wa agizo la Mahakama.
4. KUKAMATA MSHAHARA NUSU AU WOTE.
Kwa mujibu wa sheria niliyotaja hapo juu, mshahara wa mfanyakazi unaweza kukamatwa wote kwa ujumla wake au sehemu yake kutegemea na maamuzi ya Mahakama. Ikiwa deni ni kubwa sana basi inaweza kuamriwa kuwa kiasi fulani kiwe kinakatwa kila mwezi, labda kwa kipindi cha miaka miwili au mmoja kutegemea na deni lenyewe. Au kama mshahara ni mkubwa na upo uwezekano wa kulipa deni kwa mkupuo mmoja (single installment) na likaisha, basi inaweza kuamriwa mshahara ukamatwe wote na ulipie deni kwa mkupuo mmoja ili deni liishe kabisa.
Hata hivyo katika mashauri yanayohusisha familia kama matunzo ya watoto, ada, mavazi, malazi na matunzo ya mwanamke mara nyingi huwa inaamriwa kiasi fulani kila mwezi kikatwe na kiingie katika akaunti ya mwanamke au kipelekwe Mahakamani kwa ajili ya matunzo kwa familia hiyo.
5. MALIPO KUFANYIKA HATA KAMA MFANYAKAZI YUKO NJE YA MKOA.
Ikiwa kesi imefunguliwa mkoa fulani na mfanyakazi anakofanyia kazi ni mkoa mwingine, bado hili halizuii mshahara kukamatwa. Popote anapofanyia kazi na popote ofisi yake ilipo mshahara utatakiwa kukamatwa na kulipia kile anachostahili kulipia. Yote hayo ni kwa mujibu wa amri ya 21 kanuni ya 47 sura ya 33 sheria ya mwenendo wa mashauri ya madai.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE, GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment