Gari ambalo limenunuliwa kwa ajili ya kunyonya maji taka, mji wa Mbinga mkoani Ruvuma. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
HALMASHAURI ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, imeweza
kuondokana na mfumo wa kukodi gari la kunyonya maji taka kutoka Manispaa ya
Songea mkoani humo, baada ya kununua gari lake ikiwa ni mikakati yake ya
kuhakikisha kwamba wakazi wa mji huo wanaondokana na kero hiyo.
Gari hilo ambalo ni aina ya FAW lenye namba za usajili, SM
11483 limenunuliwa kwa fedha za kitanzania, shilingi milioni 164,654,000.
Akizungumza na mwandishi wetu, Mkurugenzi mtendaji
Halmashauri ya mji wa Mbinga, Oscar Yapesa alisema kuwa lengo la kununua gari
hilo ni mpango uliowekwa muda mrefu, ili kuweza kuboresha makazi na mazingira
ya mji huo kuwa katika hali nzuri.
Yapesa aliongeza kuwa, awali halmashauri hiyo ilikuwa
ikitumia gharama kubwa kukodi gari la kunyonya maji taka kutoka Songea ambapo
waliona ni vyema waweke mpango wa kununua gari lao, ili baadaye liweze
kuhudumia wakazi wa mji huo kwa gharama nafuu pale wanapohitaji huduma.
“Lengo letu ni kuendelea kuboresha huduma ndani ya mji wetu
kuwa katika hali nzuri ya usafi, kwa kuhakikisha tunasogeza miundombinu husika
karibu na wananchi, waweze kupata huduma kwa urahisi pasipo usumbufu wa aina
yoyote ”, alisema Yapesa.
Kadhalika naye Ofisa afya wa mji huo, Felix Matembo
alifafanua kuwa utawekwa utaratibu mzuri juu ya matumizi ya gari hilo na
baadaye watatoa matangazo kwa wananchi, ili waweze kujua lini litaanza kutumika
na wachangamkie fursa iliyopo ya matumizi ya mtambo huo wa kunyonya maji taka.
Pamoja na mambo mengine, Matembo aliongeza kwa kuwataka wakazi
waishio katika mji wa Mbinga kuzingatia suala la usafi hasa katika kipindi hiki
cha masika ili kuweza kuepukana na magonjwa ya mlipuko, kama vile kipindupindu
ambacho hutokana na mazingira kuwa machafu.
Alisema kuwa yeye akiwa msimamizi mkuu wa masuala ya usafi
katika mji huo, kamwe hatakubali kufumbia macho jambo hilo, badala yake anataka
kuona watu wanazingatia usafi, kinyume na hapo ameapa kwamba atakayekamatwa
anakiuka taratibu husika atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kutozwa faini
ya shilingi 50,000 au kufikishwa Mahakamani.
No comments:
Post a Comment