Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WANANCHI wanaoishi katika kijiji cha Mkako na Litoho,
Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, hawana maji safi na salama
kutokana na serikali kushindwa kukamilisha ujenzi wa miradi miwili ya maji,
iliyopo katika vijiji hivyo.
Aidha hali hiyo, imesababishwa na ukosefu wa fedha shilingi
bilioni 1,082,199,509 ambazo mpaka sasa serikali haijazipeleka katika maeneo
hayo, kwa ajili ya kuweza kufanya kazi ya ujenzi wa miradi hiyo.
Mhandisi wa maji wilaya ya Mbinga, Vivian Mndolwa alibainisha
kwamba mkandarasi husika ambaye alipewa miradi hiyo kwa ajili ya ujenzi,
amefikia kiwango cha asilimia 60 cha ujenzi na sasa imesimama kutokana na
ukosefu huo wa fedha.
“Hii miradi ni mikubwa na fedha tunategemea kupata kutoka kwa
wafadhili, hivyo imekwama ujenzi wake kutokana na sababu hiyo, hivyo tunaiomba
serikali ione namna gani ya kumaliza jambo hili”, alisema Vivian.
Vivian alifafanua kuwa ujenzi wa miradi hiyo hapo ulipofikia,
kiasi kikubwa cha fedha zilizotumika katika ujenzi wake zimetoka kwa mkandarasi
aliyepewa mradi na kwamba hivi sasa, anaidai serikali shilingi milioni
932,746,483 ili aweze kukamilisha ujenzi wa miradi hiyo.
Pamoja na mambo mengine, Mhandisi huyo wa wilaya ya Mbinga,
aliwataka wananchi wa wilaya hiyo kutunza vyanzo vya maji hasa katika maeneo
ambayo miradi ya maji, ujenzi wake umekamilika.
Alisema waache vitendo vya uharibifu wa misitu na wizi wa
mabomba ya maji ambayo yamefukiwa chini ya ardhi, kwani vitendo vya kuhujumu
miundombinu ya maji kunahatarisha ustawi wa maendeleo yao katika jamii.
“Licha ya kukamilika kwa baadhi ya miradi ndani ya wilaya
yetu, wapo baadhi ya wananchi wanakiburi, wamekuwa wakilima mashamba karibu na
vyanzo vya maji jambo ambalo ni la uharibifu wa mazingira”, alisema.
Kufuatia uharibifu huo ambao unafanywa na watu wachache, aliongeza
kwamba idara imekuwa ikichukua hatua kwa kuwaandikia barua za onyo uongozi
husika wa kijiji, ikiwa ni lengo la kuwataka wahame wasiendelee kufanya
uharibifu huo.
Vivian alieleza pia, elimu imekuwa ikitolewa kwa wananchi juu
ya utunzaji wa vyanzo hivyo ili viweze kuwa endelevu na kuzalisha maji wakati
wote, na walaji waweze kuondokana na adha ya upatikanaji wa maji safi na
salama.
No comments:
Post a Comment