Na Muhidin Amri,
Mbinga.
JUMUIYA ya Umoja wa Wanawake Chama cha Mapinduzi (UWT) wilayani
Mbinga mkoa wa Ruvuma imesema, haitawavumilia wanachama wa umoja huo ambao
walikisaliti chama katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu,
ambapo kinaweka mikakati ya kuwachukulia hatua wale wote walioonekana kwenda
kinyume na matakwa husika, ikiwa ni lengo la kulinda heshima na maadili ya
chama hicho.
Pendo Ndumbaro ambaye ni Mwenyekiti wa umoja huo wilayani humo,
alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wanachama wake katika mkutano wao, uliofanyika
ukumbi wa jumba la maendeleo mjini hapa.
Alisema baadhi ya wanachama, walishindwa kukisaidia chama
katika mchakato mzima wa uchaguzi mkuu huku wengine wakipigia debe vyama vya
upinzani, ili CCM kisiweze kupata ushindi katika uchaguzi huo.
Ndumbaro alisema kuwa wanachama vigeugeu, mara nyingi ndiyo
wanaoanzisha mizengwe na vurugu za hapa na pale ndani ya chama hali ambayo
inakiweka chama katika wakati mgumu, na kutoa nafasi kwa vyama vya vingine kuendelea
kujiimarisha hata kama havina idadi kubwa ya wanachama.
Kwa mujibu wa Ndumbaro alidai kwamba wanachama wa aina hiyo
ni hatari ndani ya chama kwa kuwa wapo kwa ajili ya maslahi yao binafsi na sio chama,
hivyo muda umefika kuwachukulia hatua ili kuepukana na kundi kubwa la
wanachama ambao ni mamluki wanaoweza kuleta mifarakano isiyokuwa ya lazima.
Alibainisha kuwa katika uchaguzi wa mwaka huu, UWT imejipanga
vizuri na kuhakikisha wale wote watakaoteuliwa kugombea nafasi za uongozi ndani
ya umoja huo, ni watu wanaokubalika ndani ya chama na kwa wananchi ili kuepusha
chama kufanya vibaya kama ilivyotokea kwa baadhi ya maeneo hapa nchini.
Hata hivyo alisema wameshaanza kuwafuatilia kimya kimya,
baadhi ya wanachama wake na iwapo watabainika kukiuka taratibu husika watachukuliwa
hatua za kinidhamu.
No comments:
Post a Comment