Friday, November 20, 2015

HAWATAKI KUONA BENDERA ZA CHADEMA ZIKIPEPEA MAHANJE

Na Mwandishi wetu,
Songea.

WANACHAMA 17 wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika kijiji cha Mahanje jimbo la Madaba wilayani Songea, wamekikimbia chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kile walichoeleza kutofurahishwa na matokeo ya uchaguzi mkuu wa udiwani, ubunge na urais katika maeneo mengi hapa nchini licha ya watu wengi kuonekana kukiunga mkono chama hicho.

Edward Lowassa.
Wanachama hao, mbali na kurudisha kadi pia waliamua kuchoma  moto bendera za CHADEMA kwa madai kwamba hawataki tena kuona bendera zake zikipepea kwa sababu zinaweza kuwarudisha,  tena katika Chama hicho.

Mbali na hilo walisema chama hicho licha ya umaarufu wake kisiasa, hata hivyo hakina sera nzuri wala mikakati thabiti inayoweza kukifanya kushinda kwani wagombea wake wengi, ambao wanajitokeza kugombea nafasi mbalimbali hawana uwezo wa kuongoza wananchi ikilinganishwa na wale wanaopitishwa na CCM.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, John Mlelwa alisema wameamua kujiunga na CCM ili kuungana nao  katika mkakati wa kuleta maendeleo ya wananchi kwani tayari hata mgombea wake wa urais, Dokta John Magufuli kwa kipindi kifupi alichokuwa madarakani ameonesha kwa vitendo,  kupigania maisha ya Watanzania hasa wale wa kipato cha chini.



Mlelwa alisema, kwa sasa hawana tena sababu ya kubaki CHADEMA kwani katika uchaguzi mkuu uliopita ambao ulifanyika Oktoba 25 mwaka huu, kimeonesha udhaifu mkubwa  kwa kuwa walitegemea kupata nafasi nyingi za ubunge na udiwani hata hivyo ni jambo la kushangaza Chama hicho, kimeendelea kuwa  msindikizaji  kwa CCM.

No comments: