Na Bashir Yakub,
UNAPOSHINDWA kesi sio mwisho wa
kusaka haki. Hii ni kwasababu kushindwa
kesi kunatokana na sababu nyingi. Si kweli
kwamba kwakuwa umeshindwa kesi katika Mahakama
fulani basi maana yake ni kuwa ulikuwa
huna haki.
Yawezekana kabisa haki ilikuwa
yako isipokuwa umeshindwa tu kutokana na
sababu nyingine za kiutaratibu na kimbinu (procedures
& technicalities). Pia waweza kuwa umeshindwa
kutokana na uwezo mdogo wa kujieleza na
kushindwa kugusa nukta muhimu ambazo
kimsingi ndizo zilizokuwa zinabeba shauri
lako.
Lakini pia waweza kuwa
umeshindwa kwasababu ya hila na mbinu
chafu. Na hii wakati mwingine huwahusisha
hata waamuzi yaani Mahakimu na majaji. Basi
ifahamike kuwa ni sababu hizi
zilizopelekea kuwepo utaratibu wa rufaa ili
yule anayehisi kutotendewa haki aende mbele
ili kuona kama anaweza kupata haki yake
huko.
1.RUFAA NI NINI
Rufaa ni hatua ya kisheria
ya kupeleka malalamiko katika hatua ya Mahakama
ya juu zaidi baada ya mmoja wa
wahusika katika kesi iliyoisha kutoridhishwa
na hukumu/maamuzi. Ili ukate rufaa ni lazime
uwe ulikuwa mhusika katika kesi iliyoisha
na uwe na sababu za kwanini unadhani
hukuridhishwa na maamuzi. Sababu yoyote ya
msingi inakubalika.
2. NI HAKI YAKO KUAMUA KUKATA
RUFAA AU KUACHA
Suala la kukata rufaa halitegemei
hisani ya Mahakama. Sio upendeleo ambao mtu
anapewa ili kuendelea kusaka haki. Ni haki
ya msingi na ya kisheria ambayo hutumiwa
na yule ambaye anahisi kutotendewa sawa
katika shauri la awali lililoisha.
Pia ieleweke kuwa rufaa tunazoongelea
hapa ni zile rufaa katika mashauri ya
madai. Rufaa katika mashauri ya madai
tunaongelea mashauri ya ardhi, ndoa, mikataba,
migogoro ya biashara na mauziano kwa
ujumla, migogoro ya madeni na yale
yote ambayo sio jinai. Kwa hiyo katika
malalamiko ya namna hiyo ni uamuzi
wako ukate rufaa kwenda mbele au uache
hata kama umeshindwa. Hii ni haki yako
na katu haiondolewi na yoyote.
3. HATA ALIYESHINDA KESI ANAWEZA
KUKATA RUFAA
Hapo juu tumesema rufaa ni kwa
mtu ambaye hakuridhishwa na maamuzi ya
Mahakama. Sio kwa ajili ya aliyeshindwa
bali ni kwa ajili ya yule ambaye
hakuridhishwa. Hii ina maana kuwa unaweza
ukashinda lakini ukawa hukuridhishwa.
Na kama umeshinda lakini hukuridhishwa
pia waweza kukata rufaa. Kwa mfano
ulifungua kesi ukiomba fidia ya milioni 50.
Hukumu ikatoka kuwa umeshinda lakini
ikasema kuwa utalipwa milioni kumi tu. Kwa
mazingira kama haya ni kuwa umeshinda lakini
waweza kukata rufaa kudai zaidi. Utakata
rufaa kwakuwa umeshinda lakini
hukuridhishwa na ushindi. Kinachotakiwa kueleweka
hapa ni kuwa rufaa inaweza kukatwa
hata yule aliyeshinda kesi na si tu
kwa aliyeshindwa.
4. NAMNA YA KUKATA RUFAA
Mara tu kesi inapoisha hakikisha
unafuatilia na kupata nakala ya hukumu
pamoja na tuzo (decree). Fuatilia kwa karani wa
Hakimu/Jaji aliyesikiliza shauri lako na umwambie
nia yako ya kutaka nakala ya hukumu
na tuzo kwa ajili ya kukata rufaa.
Huwezi kukata rufaa bila nakala ya
hukumu kwakuwa ni lazima uipitie kwa
umakini na kuona ni wapi palikuwa na
tatizo ili iwe ndiyo sababu yako ya
rufaa.
Ikiwa hukumu ilitolewa na Mahakama
ya mwanzo, basi rufaa itaenda Mahakama
ya wilaya, na ikiwa ilitolewa na Mahakama
ya wilaya rufaa itaenda Mahakama kuu
na ikiwa ilitolewa Mahakama kuu basi
rufaa huenda Mahakama ya rufaa ambayo
ni Mahakama ya mwisho kiitifaki. Pia rufaa
zinazotoka katika Mahakama za hakimu mkazi
kama ile ya kisutu ambazo baadhi huziita Mahakama
za mkoa, rufaa zake huenda Mahakama kuu
pia.
Unapokuwa unaandaa sababu za
rufaa hakikisha unamuona mwanasheria kwa
ajili ya kupitia hukumu na kukusaidia
kuandaa sababu za rufaa. Hii ni kwasababu ipo
namna ya kisheria ya kuandaa sababu hizi
kwani haziandaliwi kama barua.
Muda ni suala la msingi
sana katika kukata rufaa. Hakikisha pale tu
hukumu inatolewa unaandika barua Mahakamani ya
kuomba nakala ya hukumu. Hii itasaidia hata
zile siku 30 au 45 za rufaa
zikipita kabla hujapatiwa nakala ya hukumu
kujitetea kuwa ulichelewa kwakuwa ulikuwa
ukisubiria nakala ya hukumu ambayo uliiomba
ndani ya wakati stahiki.
MWANDISHI WA MAKALA
HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI
LA HABARI LEO KILA JUMANNE ,
GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI
NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959,
0714047241
bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment