Mtambo wa kubangua na kuchambua korosho uliopo katika kiwanda cha kubangulia korosho wilayani Tunduru, mkoa wa Ruvuma.
|
Na Steven Augustino,
SIKU zote Taifa la Tanzania limekuwa likitegemea kilimo kuwa ndio
uti wa mgongo, hivyo bila uwepo wa viwanda vya kusindika mazao
ambayo yamekuwa yakizalishwa na wakulima hao, uzalishaji wao utakuwa ni kazi
bure na hauwezi kuwaletea tija katika maisha yao.
Kutokana na uwepo wa umuhimu wa sekta ya viwanda hapa duniani
katika kukuza uchumi na kuhakikisha dhamira hiyo inatimia, umoja wa kundi la
Export Trading Group (ETG) umechukua jukumu la kupeleka fursa ya ujenzi
wa kiwanda cha kubangulia zao la korosho kwa wakulima wa wilaya ya Tunduru mkoani
Ruvuma.
Ni ukweli usiofichika kwamba, kiwanda hiki ambacho ni
tegemeo kubwa katika kuinua uchumi wa wananchi wa wilaya hiyo, hivi
sasa kimejiwekea mikakati kabambe ambayo itaenda sambamba na msimamo wa
serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dokta John Pombe Magufuli,
ambaye amekuwa akitilia mkazo wa kufufua na kujenga viwanda vipya hapa nchini,
ili kuweza kuongeza ajira.
Kiwanda hiki ambacho kinaendeshwa chini ya mwamvuli wa kundi
la (ETG) ambalo ilikinunua, wakati kinamilikiwa na serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania pale ilipojitoa katika uwekezaji mwaka 2005.
Baada ya kukamilika kwa taratibu hizo ETG, ilianza utekelezaji
wa shughuli za ubanguaji korosho kutoka kwa wakulima wa wilaya hiyo, mwezi Aprili
mwaka 2008 na kwamba hivi sasa kimekuwa tegemeo kubwa la kutoa ajira kwa wananchi
wa wilaya ya Tunduru.
Takwimu kutoka ndani ya uongozi wa kiwanda hiki, ambazo zimethibitishwa
na mhasibu wa kiwanda hicho, Niraj Patel zinaeleza kuwa jumla ya watu 700
kutoka idadi ya watu 300 wameweza kuwaajiri wakati kinaanzishwa.
Anasema mbali na mafanikio hayo na kufikia idadi ya kutoa
ajira hizo, wengi wao walioajiriwa ni wanawake ambao hivi sasa wamekuwa
wakinufaika na familia zao ambazo wanaishi nazo.
Pamoja na watu hao kuishi katika kipindi hicho na kutegemea
ajira za muda, anasema kwamba wamekuwa pia wakinufaika kutokana na kipato
ambacho hutokana na ujira huo, kwa kujiletea maendeleo.
"Sisi kama
kiwanda hatuwatazami watu 700, wanaofanya kazi katika kiwanda chetu, bali
tunawahudumia kwa kuzitazama familia zao ambazo zinawazunguka wafanyakazi
wetu", alisema Patel.
Anasema uwekezaji wa kiwanda hiki wilayani hapa, unalenga
kuongeza ajira mbadala kwa jamii pamoja na uzalishaji wa zao la korosho hapa
nchini, kuboresha upatikanaji wa soko bora na la uhakika kwa zao hilo, pamoja
na kutangaza jina la Tanzania.
"Uwekezaji
wa kiwanda chetu mbali ya kutegeneza ajira mbadala kwa jamii, pia tunalenga
kuongeza uzalishaji wa zao hili la Korosho na upatikanaji wa masoko ya uhakika ya
kuuzia zao hili", alifafanua Patel.
Shughuli zinazofanywa katika kiwanda hicho anasema kuwa
zinajumuisha ununuaji wa zao hilo, ukaushaji, ubanguaji, upangaji wa madaraja,
upakiaji na uuzaji wa korosho hizo nje ya nchi.
Katika kufikia lengo husika uongozi wa kiwanda, umekuwa
ukiangalia uwezekano wa kuanza kutoa ajira ya kudumu miongoni mwa wafanyakazi
wake, ikiwa ni juhudi ya uboreshaji wa maslahi ya wafanyakazi wake.
Naye fundi mkuu wa mitambo katika viwanda vya kubangulia zao
la korosho wilayani Tunduru, Masasi, Newala na Mtwara Injinia Sivan Edayeth
anasema pamoja na kuwepo kwa mafanikio hayo, bado wanahitaji kuendelea
kuboresha miundombinu ya viwanda vilivyopo katika maeneo hayo.
Injinia huyo anasema lengo uboreshaji huo, ni kuweza
kurahisisha uzalishaji wa korosho kuwa katika ubora wa hali ya juu na
unaokubalika.
Anasema hivi sasa mitambo iliyopo katika kiwanda cha Tunduru,
inao uwezo wa kuzalisha kiasi cha tani 4,000 katika kipindi cha misimu
tofauti na hapo awali walikuwa wakibangua tani 2500.
Utekelezaji wa shughuli zao, kiwanda hutegemea kuuza korosho katika
masoko yaliyopo katika nchi ya India, Marekani, Uingereza na zile za ukanda wa
ghuba.
Mhandisi Edayeth anawashukuru viongozi wa serikali na
wananchi wa wilaya ya Tunduru, kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakiwapatia tangu
kuanzishwa kwa kiwanda hicho.
Kadhalika msimamizi mkuu wa wafanyakazi wa kiwanda hicho,
Issa Kaesa anaeleza kuwa tangu kuanzishwa kwa kiwanda hicho kumekuwa
kukijitokeza malalamiko mbalimbali, kutoka kwa wafanyakazi wake lakini kutokana
na uhodari wa uongozi wao wamekuwa wakiyatatua na kuendelea na kazi.
No comments:
Post a Comment