Sixtus Mapunda, akizungumza na akina mama wanaosubiri kujifungua katika wodi ya wazazi iliyopo Hospitali ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma. (Picha zote na gwiji la matukio Ruvuma) |
Mbinga.
HOSPITALI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, inakabiliwa na
tatizo la ukosefu wa jengo la kisasa la upasuaji jambo ambalo wagonjwa wengi
wanaohitaji kupata huduma za upasuaji katika hospitali hiyo, hupata shida
kutokana na jengo linalotumika sasa kuwa chakavu na halikidhi mahitaji husika.
Aidha imeelezwa kuwa hospitali hiyo, haina gari la kubebea
wagonjwa ambapo hulazimika kutumia gari la kituo cha afya Mapera, kilichopo
katika kata ya Mapera wilayani humo.
Sixtus Mapunda ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini,
alielezwa hayo leo alipokuwa katika ziara ya kutembelea hospitali hiyo ya
wilaya Mbinga kwa lengo la kujionea changamoto mbalimbali, ambazo hospitali hukabiliana
nazo.
Aliweza kutoa mchango wa vifaa tiba kama vile dawa za
kufanyia usafi, bandeji za kufungia na kusafishia vidonda na mipira ya kuvaa
mikononi (Gloves).
Vilevile aliwapatia akina mama wajawazito na waliojifungua
watoto ambao wapo wodini wamelazwa; sabuni za kuogea, miswaki na dawa za kusafishia
meno ikiwa ni lengo la kuboresha afya zao ziweze kuwa katika hali nzuri.
Mbunge huyo ambaye aliambatana na mkewe, Jiang Alipo
walikutana na changamoto kadhaa ambazo hospitali hiyo hukabiliana nazo, ikiwemo
uchakavu wa majengo hasa la akina mama hao wajawazito na wagonjwa mahututi
(ICU).
Akisoma taarifa fupi juu ya maendeleo ya hospitali ya wilaya
ya Mbinga, Mganga mkuu wa halmashauri ya mji wa Mbinga, Dokta Elisha Roberth
alisema kuwa jengo la kulaza wagonjwa daraja la kwanza lililopo katika hospitali hiyo, hasa kipindiki hiki cha masika linavuja na kwamba
linahitaji ukarabati mkubwa ili liweze kuwa katika hali nzuri.
“Licha ya kuwepo na changamoto nyingi zinazotukabili, wodi ya
wazazi pia ni chakavu inahitaji ukarabati ili hata mbu ambao huingia katika madirisha
ambayo ni mabovu na kuleta madhara kwa wagonjwa, wasiweze kuendelea kuleta
matatizo”, alisema Dokta Elisha.
Dokta Elisha alizungumzia pia tatizo la uhaba wa watumishi,
alisema kuwa wagonjwa wanaotakiwa kupatiwa matibabu ni wengi hivyo kuna kila
sababu kwa serikali kuona namna ya kutatua tatizo hilo, ili wagonjwa waweze
kupatiwa huduma ipasavyo.
“Upungufu wa watumishi nilionao ni mkubwa hasa kwa kada ya madaktari,
wagonjwa tunaowapokea kwa siku ni wengi hufikia idadi ya 180 hadi 210 lakini
tunafanya jitihada pamoja na upungufu wa watumishi tulionao tunatekeleza
majukumu tunayopaswa kuyatekeleza”, alisema.
Pamoja na mambo mengine, Mganga huyo aliongeza kuwa kumekuwa
na tatizo la kutokuwepo kwa jengo la kutolea huduma wagonjwa wenye matatizo ya
akili ambapo hivi sasa hulazimika kulaza wagonjwa wenye matatizo hayo, katika
wodi za wagonjwa wengine wa kawaida jambo ambalo wakati mwingine waganga
wanaokuwa zamu kutibu wagonjwa wodini, huogopa na kutotimiza majukumu ya kazi zao
ipasavyo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini, Sixtus
Mapunda baada ya kupokea changamoto hizo aliahidi kujenga ushirikiano kati ya uongozi
wa halmashauri ya wilaya hiyo (serikali) na wadau mbalimbali, juu ya kutatua
kero hizo na hatimaye wananchi waweze kupata huduma kikamilifu.
“Ni lazima tujenge ushirikiano mkubwa ili tuweze kutatua
matatizo haya yaliyopo mbele yetu, tusitegemee wakati wote tupate mahitaji
kutoka wizara ya afya naomba tushirikiane ili tuweze kutimiza malengo husika”,
alisema Mbunge huyo.
Hata hivyo, Mapunda alisema yeye anatambua kwamba sekta ya
afya inakabiliwa na changamoto nyingi hivyo amewataka wafanyakazi wote kwa
ujumla wao waliopo katika hospitali ya wilaya ya Mbinga, kutekeleza wajibu wao
ili kuweza kutimiza matakwa husika ya wananchi na kuondoa malalamiko yasiyokuwa
ya lazima miongoni mwa jamii.
No comments:
Post a Comment