Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MBUNGE wa Viti maalum mkoani Ruvuma, Jacqueline Msongozi
amezitaka Halmashauri za wilaya mkoani humo kutekeleza jukumu la kupeleka
asilimia 10 ya fedha za mapato yake ya ndani katika vikundi vya ujasiriamali, kwa
wanawake na vijana.
Aidha amewaagiza madiwani wa mkoa huo, kuhakikisha kwamba
suala hilo wanalifuatilia kwa karibu ndani ya Halmashauri zao kupitia vikao
husika, ili fedha hizo zielekezwe kwa kundi hilo.
Msongozi alitoa agizo hilo, alipokuwa akizungumza na akina
mama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) tawi la Mbinga, katika kikao cha
baraza la wanawake kilichofanyika kwenye ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliopo
mjini hapa.
Mbunge huyo alisema kuwa wanawake wanaweza kujituma kwa kila
jambo la kimaendeleo, hivyo wanapaswa wakati wote kutetea haki zao pale wanapoona
zinaporwa na watu wasiopenda maendeleo yao.
“Madiwani mliochaguliwa nawataka pia mrudi kwenye kata zenu
kutumikia wananchi na sio muda mwingi kuwa mbali, tabia ya kutengeneza majungu
na fitina tuache sasa tuunge mkono kauli mbiu ya Rais wetu John Magufuli, ‘Hapa
kazi tu’ kwa kufanya kazi kwa ushirikiano kwa maendeleo ya taifa letu”, alisema
Msongozi.
Vilevile aliwataka wanawake kujiunga katika vikundi vya
ujasiriamali, ili waweze kujikwamua katika maisha yao ya kila siku na sio muda
mwingi kulalamika na kukaa bila kujishughulisha.
Akizungumzia juu ya suala la elimu, Msongozi alisema kuwa
watoto wote waliomaliza darasa la saba mwaka huu, wazazi wao wahakikishe
wanawapeleka shule kwa ajili ya kuanza kidato cha kwanza na sio kuwaacha
nyumbani au mitaani wakiwa wanazurula hovyo na kujifunza matendo maovu kama
vile uvutaji wa madawa ya kulevya.
“Ndugu zangu ona fahari kuona kwamba, mtoto wako anapata
elimu na sio kumtumikisha kwa kufanya kazi za kuchunga ng’ombe au mbuzi tuone
kwamba ni wajibu wetu watoto hawa, mwisho wa siku wanakuwa na elimu ya kutosha”,
alisema.
No comments:
Post a Comment