Na Muhidin Amri,
Mbinga.
MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga
amewataka wananchi wa wilaya hiyo kutumia mvua zinazoendelea kunyesha katika
msimu wa mwaka huu, kwa kupanda miti kwa wingi ili kujiongezea
kipato baada ya kuonekana zao hilo ni miongoni mwa vyanzo vikubwa vya kukuza mapato
na uchumi, kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Senyi Ngaga. |
Aidha aliwataka waache tabia ya kukata miti hovyo
na kuchoma moto misitu hasa nyakati za kiangazi kipindi wanapoandaa mashamba yao,
kwa ajili ya shughuli za kilimo huku akiongeza kuwa tabia hiyo imekuwa
ikisababisha uharibifu wa mazingira na virutubisho vya udongo hupotea.
Ngaga alitoa wito huo mwishoni mwa wiki, alipokuwa
akizungumza na wananchi wa kijiji cha Amani Makolo wakati walipokuwa katika kazi
ya upandaji miti, kata ya Amani Makolo wilayani humo.
Alisema kuwa changamoto kubwa ya uharibifu wa
mazingira, imejitokeza katika maeneo yanayozalishwa kwa wingi zao la mahindi na
kwenye misitu ya asili, kasi ya ukataji miti na uchomaji moto ni kubwa.
Kadhalika
aliwaagiza maofisa tarafa, kushirikiana na watendaji wa kata na vijiji
kuhakikisha wanawachukulia hatua wale wote wenye tabia ya kukata na kuendesha
shughuli za kilimo na ufugaji kwenye maeneo ya vyanzo vya maji, na endapo wataachwa
bila kuwachukulia hatua huenda likatokea tatizo kubwa la upotevu wa vyanzo
hivyo.
“Niwaombe wananchi waache kulima kwenye vilele
vya milima na vyanzo vya maji, kumbukeni maji ni uhai na tegemeo kwa viumbe
vyote hai na vile visivyo hai hivyo naagiza kila kijiji kihakikishe kinafuata
taratibu na sheria ndogo zitakazosaidia kuwabana wale wote wanaojihusisha na
uharibifu wa mazingira”, alisisitiza.
Awali katika taarifa yake Ofisa misitu wa wilaya
hiyo, Vicent Mwafute alisema kuwa lengo la wilaya hiyo ni kukuza miche milioni
3,500,000 kila mwaka na kwamba kuanzia mwaka 2010 mpaka kufikia mwezi Disemba
mwaka jana, jumla ya miche milioni 11,386,648 imekuzwa na kupandwa kwa hekta
6,325 sawa na asilimia 90 ya upandaji.
Mwafute alisema changamoto zinazoikabili wilaya ya
Mbinga, katika kutekeleza mpango huo wa kupanda miti kila mwaka ni pamoja na elimu
ya uhifadhi wa mazingira, upandaji miti na kuitunza kama mazao mengine ambapo bado
wananchi hawajaipokea kikamilifu na kwamba ili kufanikisha hilo serikali, wananchi
na taasisi mbalimbali kwa ujumla wilayani humo zinapaswa kujitoa kwa moyo wa dhati
na kuwekeza katika shughuli za upandaji miti.
No comments:
Post a Comment