Na Julius Konala,
Songea.
WAENDESHA pikipiki maarufu kwa jina la boda boda, Manispaa ya
Songea mkoani Ruvuma, wamempongeza Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Dokta John Magufuli kutokana na utendaji kazi wake imara na
shupavu.
Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa waendesha boda boda
Manispaa ya Songea mkoani humo, Abeid Nchimbi kwa niaba ya wenzake alipokuwa
akisoma risala yao mbele ya mgeni rasmi Mbunge wa jimbo la Songea mjini
Leonidas Gama, ambalo lilipambwa na maandamano ya pikipiki kutoka Ruhuwiko na
kisha kupokelewa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali, kwenye uwanja wa
michezo Majimaji uliopo mjini hapa.
Leonidas Gama. |
Nchimbi alisema kuwa wameamua kumuunga mkono kutokana na
jitihada zake anazo zionesha katika kupambana na vita dhidi ya rushwa, ufisadi,
matumizi mabaya ya fedha za serikali, wanaokwepa kulipa kodi pamoja na kukamua
majipu mengine mbalimbali.
Aidha alisema kuwa kutokana na imani kubwa aliyoionesha Dokta
Magufuli kwa Watanzania, hivyo wao kama vijana wameamua kuvunja makundi
mbalimbali yaliyokuwa miongoni mwao na kuamua kujiunga katika vikundi vidogo
vidogo vya uzalishaji na ujasiriamali, kwa lengo la kujikwamua na hali ngumu ya
maisha.
Akizungumza katika tukio hilo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) wilaya ya Songea mjini, Gerlod Mhenga amewataka vijana hao kuendelea
kukiunga mkono chama hicho na kumuomba Mbunge wa jimbo la Songea mjini,
Leonidas Gama kuhakikisha anatekeleza ahadi mbalimbali alizowaahidi wananchi wake,
wakati wa kampeni zilizopita za uchaguzi mkuu ikiwa pamoja na kutoa mikopo
katika vikundi vya akina mama na vijana, hususani kwa hao waendesha boda boda.
Naye Mkuu wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Benson Mpesya amewapongeza
vijana hao kwa kuendelea kufanya usafi wa mazingira, kuzoa taka kwenye maghuba
mbalimbali huku akiwataka waendelee na moyo huo wa kizalendo.
Kwa upande wake Mbunge huyo wa jimbo la Songea mjini kupitia
tiketi ya CCM alisema, atahakikisha akina mama na vijana wanapatiwa mikopo yenye
riba nafuu kwa lengo la kupanua ajira, kuongeza mzunguko wa fedha na kuimarisha
uchumi wao huku akiwataka kuendelea kumuunga mkono Dokta Magufuli kwa kufanya
kazi halali kwa juhudi na maarifa, kuwafichua mafisadi, majambazi na kufuata
sheria za usalama barabarani.
No comments:
Post a Comment