IRINGA.
ZAIDI ya vijana 50 wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Iringa mjini,
wanaojiita “wafia chama” kwa zaidi ya saa mbili juzi waliwafungia ndani ya Ofisi
za Chama hicho mkoa wa Iringa wajumbe wa kamati ya siasa ya mkoa huo, akiwemo na
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu wakishinikiza aachie
ngazi.
Msambatavangu anatuhumiwa na baadhi ya makada wa chama hicho,
kukihujumu chama jimbo la Iringa mjini wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika
Oktoba 25 mwaka huu, jambo walilosema limesababisha wapoteze kata 14 kati ya 18
na jimbo hilo kwa mara nyingine tena, kwenda kwa Mchungaji Peter Msigwa wa
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Wengine waliokutwa na kadhia hiyo ni pamoja na Mkuu wa mkoa
wa Iringa, Amina Masenza, Kaimu Katibu wa CCM mkoa wa Iringa Elisha Mwampashi,
Katibu Mwenezi wa CCM mkoa wa Iringa, Dokta Yahaya Msigwa na Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Wazazi mkoa wa Iringa, Ephraim Mhekwa.
Wengine ni pamoja na aliyekuwa Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Mufindi Kaskazini, Mahamudu Mgimwa na
aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kilolo, Joseph Muhumba.
Mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza aliyefika kikaoni hapo
kwa kuchelewa alijikuta akiingia katika kundi la wajumbe waliofungiwa katika
ofisi hizo baada ya kuwaomba vijana ha,o wafungue geti la kuingilia na kutokea
katika ofisi hizo zilizopo ghorofa ya kwanza ya jengo hilo.
Baada ya kufungua geti hilo, huku wakimuahidi mkuu wa mkoa
huyo kutoondoka katika ofisi hizo mpaka watakapojiua nini kitafanywa na
viongozi wa chama hicho kama Mwenyekiti huyo wa CCM mkoa wa Iringa hataachia ngazi
kwa hiari yake mwenyewe, walifunga tena geti hilo mara tu baada ya Masenza kuingia
ndani katika ofisi hizo.
Wakiwa wamefungiwa ndani, makachelo wa Polisi na wale kikosi
cha kutuliza Ghasia (FFU) wakiwa katika gari tatu za polisi aina ya Landrover
waliwasili katika ofisi hizo zilizopo jirani na stendi kuu ya mabasi, yaendeyo
mikoani kwa lengo la kuwadhibiti vijana hao.
Baada ya askari hao kufika, vijana waliokuwa na funguo za
geti hilo walipandisha haraka ghorofani na kufungua geti hilo kabla Kaimu
katibu wa CCM mkoa wa Iringa na katibu mwenezi wake, hawajatoka na kuzungumza
nao.
“La kwanza niwapongezeni kwamba mnakipenda chama na mnapenda
chama kipate ushindi, pili niwapongezeni mnauchukia usaliti ndani ya chama.
Tatu lazima mfahamu kwamba kuna vikao vinapaswa vijadili suala la usaliti, hoja
yenu ni ya msingi,” alisema Mwampashi.
Naye Dokta Yahaya alisema uongozi wa chama hicho mkoa,
umepokea taarifa za usaliti toka ngazi ya chini na mchakato wa kuzijadili
umeanza na akawaomba vijana hao kama wananyongeza wawasilishe, katika kikao
hicho cha kamati ya siasa ya mkoa.
Akizungumzia tuhuma wanazomuhusisha nazo Mwenyekiti wa CCM wa
Mkoa, mmoja wa vijana hao Salum Mbungu ambaye ni Katibu wa vijana kata ya Ruaha
na Katibu wa makatibu wa vijana wa kata zote 18 za jimbo la Iringa mjini
alisema;
“Tunataka Mwenyekiti wa mkoa ajiuzulu kwa hiari yake, kuna
ushahidi tosha unaomuhusisha yeye binafsi na baadhi ya vijana wa CCM kukihujumu
chama wakati wa uchaguzi mkuu,” alisema.
Mbungu alisema wanao ushahidi unaoonesha kiongozi huyo
alikuwa akiwashawishi baadhi ya wana CCM kuwachagua wagombea kupitia Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo kwa kile alichoeleza kuwa alikuwa mpiga debe maarufu wa
Waziri mkuu aliyejiuzuru, Edward Lowassa wakati akiwa katika mchakato wa
kuwania urais kupitia CCM.
Akizungumzia tukio hilo baada ya vijana hao kuombwa
kutawanyika huku wakihakikishiwa kwamba hoja zao zinafanyiwa kazi katika vikao
husika, Msambatavangu alisema;
“Tuhuma zinazotolewa na vijana hao na wana CCM wengine dhidi
yake sio za kweli, zinalenga kuchafua hadhi yake na kuficha ukweli wa sababu
zilizosababisha wapoteze jimbo hilo”.
Alisema tuhuma zinazotolewa dhidi yake ni za kupangwa na
zinafanywa na Katibu wa CCM wa mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga kwa maslahi yake
binafsi ili ashindwe kusimamia shughuli za chama kwa kuzingatia katiba, kanuni
na taratibu.
“Mimi siwezi kujiuzulu kwa shinikizo la kikundi cha vijana
wanaotumiwa vibaya. Tuna utaratibu wa kufanya tathimini za uchaguzi, kuanzia
ngazi ya chini hadi mkoa, ngazi ya mkoa ukishachambua unapeleka Taifa na
maamuzi yanafanyika,” alisema.
Alisema wanaomtuhumu kwamba yeye ni msaliti wanajua sababu
nyingi, kwa kuwa zinajulikana, za kwanini walishindwa uchaguzi katika jimbo la
Iringa Mjini pamoja na kutumia nguvu kubwa.
Alisema anao ushahidi wa kina na wa kutosha wa jinsi kiongozi
mwenzake huyo wa mkoa anavyoratibu mipango ya kumchafua kwa kutumia baadhi ya
vijana hao ili kuficha ukweli huo.
“Nataka niwaambie watanzania wazaziwazi kwamba kama mimi
nilikisaliti chama eti kwasababu nilikuwa Timu Lowassa hiyo ni hoja ya kipuuzi
kabisa. Ndani ya CCM kuna demokrasia inayowapa fursa wanaCCM kumuunga mkono
mgombea wanayemtaka, na hiyo hawezi kusababisha sisi tuitwe wasaliti, utaratibu
huo upo toka enzi za Nyerere,” alisema.
Alisema wakati wa mchakato wa kutafuta mgombea urais wa CCM,
Lowassa aliungwa mkono na zaidi ya robo tatu ya wajumbe wa halmashauri kuu,
zaidi ya wenyeviti 16 wa mikoa na viongozi na wanachama wengine mbalimbali
kwasababu demokrasia hiyo inawaruhusu.
Alisema pamoja na Lowassa kuungwa mkono na kundi kubwa
alijitoa CCM na kujiunga na Chadema, waliomfuata walikuwa wachache sana na hiyo
haina maana kwamba waliobaki CCM ni wasaliti.
“Nimeanza kupigwa vita muda mrefu, na vita hii ilianzia
kwenye mchakato wa kupata mgombea ubunge jimbo la Iringa Mjini kwasababu mimi
nilikuwa mmoja wa wagombea ambaye nilipigwa vita na baadhi ya viongozi, vita
hiyo inaendelea kwakuwa mgombea waliyemtaka ameshindwa na wanafanya hivyo
wakitafuta kujikosha kwasababu waliwahakikishia wana Iringa kwamba ni lazima
watakomboa jimbo la Iringa Mjini,” alisema.
Alisema amepeleka taarifa makao makuu ya chama ya jinsi
anavyohujumiwa na kupakwa matope kwa tuhuma za uongo na kwamba yupo tayari
kutoa ushahidi wa kutosha pindi atakapotakiwa kufanya hivyo ili kusafisha jina
lake.
“Leo imefika mwisho, nataka niseme kama mwenyekiti
niliyechaguliwa na wilaya zote za mkoa wa Iringa; hujuma hizi zisizo na
ushahidi, hazivumiliki na zinachosha; nasema kama kuna mtu anatumia uongo,
uzushi na majungu kutaka mimi ning’oke, kabla sijang’oka Mungu atajibu,”
alisema.
Alisema hatishwi wala haogopi mipango inayofanywa na vijana
hao, na hata kama wana mpango wa kumua, wamuue, lakini wajue historia itawahukumu
kwasababu kazi anayofanya ya kukijenga chama hicho na nguvu aliyotumia kwenye
kampeni za CCM mkoa mzima kwa kutumia rasilimali zake wanazijua.
Alisema inashangaza wanayemuita msaliti (yeye) ilikuwaje
wakamvumilia katika kipindi chote cha miezi miwili ya kampeni na kuja
kumutuhumu baada ya uchaguzi kufanyika na kupokeza jimbo.
“Inawezekanaje katika miezi miwili ya kampeni, Jesca
akaushinda uongozi mzima wa mkoa, uongozi wa vijana, uongozi wa wanawake,
uongozi wa wazazi, viongozi na wanachama wa kata na matawi, na akavumiliwa
katika kipindi chote hicho, kama hoja hizo sio za kipuuzi,” alisema.
Alisema vijana hao wakiendelea kutumiwa wajue kabisa kwamba
hawatakuwa wanafanya kazi ya kukinusuru chama na akawataka wakae chini,
watafakari na wajipange upya kwa kutumia ngazi zote za chama kujipanga upya.
Akizungumza kwa njia ya simu na mtandao huu kutoka Ludewa
mkoani Njombe, Katibu wa CCM mkoa wa Iringa, Mtenga alikanusha kuhusika na
njama zinazodaiwa na mwenyekiti wake huyo.
"Hicho kikao wameitisha wenyewe, mimi sipo Iringa,
ninawezaje kuhusika na mambo yaliyokuwa yakiendelea katika kikao walichoitisha
wao wenyewe, sitendewi haki na kimsingi sina sababu ya kufanya hayo
yanayodhaniwa nayafanya", Mtenga alisema.
No comments:
Post a Comment