Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MBUNGE wa Jimbo la Mbinga mjini, Sixtus Mapunda amewataka Vijana
wa jimbo hilo wakae na kutambua kwamba muda wa kampeni na siasa umekwisha,
kilichobaki wanapaswa kushirikiana na kutengeneza mustakabali wa maendeleo yao
na taifa kwa ujumla.
Sixtus Mapunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini. |
Aliwaonya pia wakiendelea kuwa na akili za kugombana na
kujengeana chuki kutokana na mambo ya kisiasa, hawatafika mbali badala yake
watarudi nyuma kimaendeleo.
“Niliona kuna sababu ya mimi kutafuta muda wa kukaa na
kuzungumza na vijana, mkiendekeza akili za kugombana au kupigana kutokana na mambo
ya kisiasa hizi ni akili za matope, tutumie muda wetu kujadili maendeleo yetu
wapi tulipo na wapi tunapaswa kwenda”, alisema.
Mapunda alisema hayo leo katika kikao maalumu cha vijana, ambacho
kiliketi kwenye ukumbi wa Umati uliopo Mbinga mjini na kuongeza kuwa sababu kuu
ya kuzungumza na vijana hao, ni kuchukua mawazo yao ambayo yana manufaa kwa
wananchi ili aweze kuyapeleka katika ngazi husika serikalini na yaweze
kufanyiwa kazi.
Alifafanua kuwa mfumo huo wa kuzungumza nao utakuwa endelevu
katika kipindi chote cha miaka mitano ambacho atatawala ndani ya jimbo hilo,
huku akieleza kuwa vijana ndiyo nguzo muhimu katika taifa hili ambao wanaweza
kugusa mambo ya msingi na kuisukuma serikali, iweze kuyatekeleza.
Katika kikao hicho wakichangia hoja mbalimbali kwa nyakati
tofauti, David Ndimbo na Zidadu Rashid walipongeza jitihada zilizofanywa na
Mbunge huyo kuwakutanisha vijana pamoja na kumtaka akae na wataalamu wa idara
ya ardhi wa Halmashauri ya mji wa Mbinga, kuona namna gani wataweza kumaliza
migogoro ya ardhi ambayo ipo katika mji huo.
Walisema kuwa wataalamu hao wamekuwa na kawaida ya kuingia
katika mashamba ya watu katika mji huo na kuanza kuyapima, bila kushirikisha
wananchi jambo ambalo likiendelea linaweza kuleta mifarakano isiyokuwa ya
lazima.
Vilevile walimtaka Mbunge huyo, ahakikishe kwamba mtambo
unaotumika kujenga barabara (Greda) ambao ni mali ya Halmashauri hiyo uwe
unafanya kazi ya kutengeneza barabara za mitaa mbalimbali iliyopo mjini hapa na
wananchi waweze kuondokana na kero iliyopo, ya ubovu wa barabara hizo.
Pamoja na mambo mengine Mbunge huyo wa jimbo la Mbinga mjini,
Mapunda alisema kuwa matatizo na kero mbalimbali amezipokea na atakwenda
kuzifanyia kazi ili kuweza kuondoa sintofahamu inayoendelea kuleta bughudha
miongoni mwa jamii, ili wananchi wake waweze kuishi kwa amani na utulivu.
No comments:
Post a Comment