Na Muhidin Amri,
Songea.
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma, linamshikilia Muuguzi msaidizi
wa Zahanati ya kijiji cha Utwango wilaya ya Namtumbo mkoani humo, Agnera Luena
kwa tuhuma ya kuuza dawa za serikali katika duka la mtu binafsi kinyume
cha sheria.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Revocatus Malimi
alisema tukio hilo lilitokea Disemba 23 mwaka huu majira ya saa nne asubuhi
ambapo mtuhumiwa huyo akiwa kazini, aliiba dawa hizo na kwenda kuuza katika
duka la Esha Tendwa lililopo katika kijiji cha Lusenti wilayani humo.
Revocatus Malimi. |
Alisema mara baada ya kumkamata, Polisi walifanya
upekuzi katika duka ambalo dawa hizo ziliuzwa na kukamata aina mbalimbali ambazo
ziliibwa na mtuhumiwa huyo.
Kamanda Malimi alizitaja dawa zilizokutwa katika duka hilo ni,
Paediatric cough Syrup chupa 13, Doxycline capsules kopo moja, Cotrimazole
Syrup mbili, Diazepam Tables kopo moja, PPF injection moja na Amoxiline Oral Suspension
mbili.
Aidha alizitaja dawa nyingine kuwa ni, Aspi -m-
Chlorphenamine tablets moja, Alu 1x6 Packet 4, Alu 3x6 Packet 4, ambazo thamani
yake bado haijajulikana.
Kamanda Malimi alifafanua kuwa mmiliki wa duka hilo, pia
anashikiliwa kwa tuhuma hizo na muda wowote upelelezi utakapokamilka watafikishwa
Mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi
mkoani Ruvuma, kuendelea kutoa ushirikiano kwa kuwafichua wafanyakazi wa hospitali
ambao wanajihusisha na vitendo hivyo viovu, kinyume na taratibu za kazi zao
ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria na iwe fundisho kwa wengine wenye
tabia kama hiyo.
No comments:
Post a Comment