Na Muhidin Amri,
Songea.
SHULE ya sekondari Mahanje iliyopo katika kata
ya Mahanje wilayani Songea mkoa wa Ruvuma, inakabiliwa na uhaba mkubwa wa
vyumba vya madarasa jambo ambalo linatishia watoto walioteuliwa kuanza kidato
cha kwanza kwa mwaka wa masomo 2016, kukosa mahali pa kusomea.
Kwa sasa shule hiyo ina vyumba vinne vya
madarasa kati ya 10 ambavyo vinahitajika ili viweze kutosheleza wanafunzi watakaoingia
shuleni hapo kwa ajili ya kuanza masomo ya kidato cha kwanza hadi cha nne.
Aidha kutokana na hali hiyo, baadhi ya wadau
wameanza kujitokeza akiwemo Mbunge wa jimbo la Madaba Joseph Mhagama aliyetoa
bati 130 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa, katika
shule hiyo.
Mbunge huyo amewataka wakazi wa jimbo
hilo, kujitokeza kwa wingi kuchangia nguvu zao ili kuweza kukamilisha ujenzi wa
vyumba hivyo madarasa.
Ametoa wito kwa kamati ya shule sekondari
Mahanje, walimu na baadhi ya watumishi wa Halmashauri hiyo kujenga ushirikiano
wa pamoja kwa kuhimiza pia wananchi kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo
jimboni humo.
Vilevile alibainisha kuwa kuna baadhi ya vijiji
ambavyo vimekosa maendeleo kwa sababu wananchi wake, kutofanya kazi kwa bidii
na hata kuchangia shughuli za maendeleo katika jamii.
Licha ya jimbo hilo kuwa na ardhi kubwa
inayofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali, alisema kuwa bado kuna baadhi
ya watu wanakabiliwa na umaskini unaotokana na kutofanya kazi za kujiongezea
kipato na ndiyo maana wengine wanashindwa kumudu hata mlo mmoja kwa
siku, kutokana na uvivu walionao.
Mhagama aliongeza kuwa, muda wa kuzungumzia
mambo ya siasa umekwisha na kilichobaki sasa wananchi wanapaswa kuungana na
viongozi wao kufanya kazi za mendeleo, chini ya kauli mbiu ya ‘hapa
kazi tu’, badala ya kutumia muda wao kukaa vijiweni na kufanya starehe
ambazo zinawagharimu katika maisha yao.
Kwa mujibu wa Mbunge huyo ni kwamba, dawa
ya kumaliza umaskini wanayo wananchi wenyewe kwani wanachotakiwa
kufanya ni kujituma kwa moyo mmoja na kujikita zaidi kufanya
kazi kwa kushirikiana na watendaji na madiwani wao katika kuibua na kutekeleza
miradi, kwenye maeneo yao ambayo itawawezesha kupata huduma bora katika maeneo
yao.
No comments:
Post a Comment