Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
IMEBAINIKA kuwa, Mamlaka ya maji safi na Usafi wa Mazingira
(MBIUWASA) katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, inashindwa kutimiza
mahitaji halisi ya utoaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wateja waliopo katika
mji huo, kutokana na miundombinu iliyopo kuwa chakavu.
Vilevile uzalishaji wa maji safi na salama kwa sasa katika
mji huo ni mita za ujazo 2,100 kwa siku, ikilinganishwa na mahitaji halisi yanayotakiwa
kuzalishwa ni mita za ujazo 3,640 kwa siku ambapo Mamlaka hiyo inashindwa
kufikia malengo hayo, kutokana na tatizo hilo linalowakabili.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu umebaini kuwa mji wa
Mbinga, una wakazi 43,674 kati ya hao wakazi 26,204 wanaishi katika eneo
lilipopita bomba la usambazaji maji huku maeneo mengine yaliyo pembezoni mwa
mji, yakiwa hayana mtandao wa maji safi na salama.
Mji huo kwa sasa ambao unakua kwa kasi kiuchumi na ongezeko
la watu likizidi kukua, idadi ya wateja wanaopata maji hayo hivi sasa ni 2,075
kiasi ambacho ni kidogo, tofauti na idadi halisi ya wakazi wanaoishi katika mji
huo.
Katika kuleta ufanisi mzuri wa utoaji wa huduma hiyo kwa
walaji na utekelezaji wa kazi za kila siku za MBIUWASA, kuna kila sababu kwa
mamlaka hiyo kufanya marekebisho ya bei za maji ikiwemo kupandisha bei za
huduma ili iweze kukusanya mapato ya kutosha, yatakayoweza pia kumudu gharama
za uendeshaji na uboreshaji wa miundombinu husika ili huduma ya maji iweze
kuwafikia idadi kubwa ya wananchi ipasavyo.
Meneja wa Mamlaka hiyo, Patrick Ndunguru alipotakiwa kutoa
ufafanuzi juu ya hali hiyo alithibitisha hilo na kueleza kuwa hali ya
ukusanyaji mdogo wa mapato yatokanayo na maji, kunasababisha washindwe kupeleka
huduma ya maji maeneo yasiyofikiwa na mtandao wa bomba kutokana na mji kukua
kwa kasi ikilinganishwa na kasi ya upelekaji huduma.
Alisema kuwa tatizo jingine linalowakabili kushindwa
kukarabati mabomba ambayo mengi kwa sasa ni chakavu, huvuja na kupoteza maji
kwa wingi pamoja na kushindwa kubadilisha dira za maji zilizokwisha muda wake
wa matumizi jambo ambalo linasababisha zishindwe kufanya kazi na kuisababishia
taasisi hiyo hasara.
“Tunashindwa hata kupandisha kiwango cha mishahara kwa
watumishi wetu wa mamlaka na kulipa madeni kwa wakati, kwa wazabuni wetu ambao
hutusambazia vifaa kwa ajili ya kuboresha huduma ya usambazaji maji katika mji
wa Mbinga”, alisema Ndunguru.
Ndunguru alisema kuwa, endapo bei za maji hazitarekebishwa
athari yake ni kwamba huduma zitaendelea kudorola kadiri siku zinavyozidi
kusonga mbele hivyo Mamlaka ya maji safi na Usafi wa Mazingira katika mji wa
Mbinga, hivi karibuni ilishirikisha Wadau husika wa mji huo kwa kufanya mkutano
na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na kwamba michakato
ya kuliweka sawa jambo hilo, inaendelea ili jamii hapo baadaye iweze kupata
huduma bora ya maji safi na salama na kuepukana na athari mbalimbali.
No comments:
Post a Comment