Na Julius Konala,
Songea.
MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wamefanya
uchaguzi na kumpata mstahiki Meya mpya, Alhaj Mshaweji Abdul Hassan atakayeiongoza
Manispaa hiyo kwa kipindi cha miaka mitano.
Uchaguzi huo ulifanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa
Manispaa hiyo, chini ya Mwenyekiti wake wa muda, Juma Ally ambaye ni Katibu
tawala wa wilaya ya Songea na kuhudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo wabunge, viongozi
wa vyama vya siasa, serikali, madiwani na wananchi kutoka kata zote za Manispaa
ya Songea.
Baada ya uchaguzi huo kufanyika Mwenyekiti huyo wa muda, alimtangaza
Alhaj Mshaweji Abdul Hassan wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mstahiki meya wa
Manispaa hiyo baada ya kushinda kwa kura 26 kati ya 30, dhidi ya mpinzani wake
kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mussa Ndomba ambaye alipata
kura 4.
Aidha katika uchaguzi huo, alimtangaza Consolata Kilowoko
kupitia tiketi ya CCM kuwa mshindi nafasi ya Naibu meya kwa kupata kura 25 kati
ya 30 huku mgombea wa CHADEMA, Martin Mlata akiwa amepata kura 5.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu ambaye
alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa baraza jipya la Madiwani wa Halmashauri
ya Manispaa ya Songea, aliwataka madiwani na watumishi wa Manispaa hiyo
kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano kwa kufanya kazi ya kusimamia
mapato na matumizi ya Halmashauri hiyo kwa weledi, uaminifu na uadilifu mkubwa.
Mwambungu ameonya pia madiwani na watumishi wazembe ambao
wanafanya vitendo vya ubadhirifu na rushwa, kwa madai kuwa vinasababisha miradi
mingi ya maendeleo ya wananchi kujengwa chini ya kiwango na kuisababishia
serikali hasara, ambapo alisema serikali haitamfumbia macho mtu yeyote
atakayebainika kutenda kosa hilo.
Awali akizungumza katika kikao hicho mstahiki Meya wa
Manispaa ya Songea, Alhaj Mshaweji Abdul Hassan aliwashukuru madiwani kwa
kumchagua kwa kura nyingi, kuwa kiongozi wao huku akiwataka kumpa ushirikiano
katika kulisukuma gurudumu la maendeleo ya Manispaa hiyo, bila ya kujali
itikadi ya vyama vya siasa.
No comments:
Post a Comment