Na Steven Augustino,
Tunduru.
MADIWANI wa Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma,
wamemchagua Diwani wa kata ya Mchoteka, Mbwana Mkwanda Sudi kutoka Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kuwa Mwenyekiti wao wa Halmashauri hiyo, ili aweze kuwaongoza katika
kipindi cha miaka mitano.
Aidha katika uchaguzi huo madiwani hao, pia walimchagua
Diwani wa kata ya Namakambale kupitia tiketi ya CCM, Mfaume Wadali Khalifa
kuwa makamu wa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo.
Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma. |
Matokeo ya uchaguzi huo, yalitangazwa kwenye ukumbi wa Klasta
ya walimu tarafa ya Mlingoti iliyopo mjini hapa.
Msimamizi wa uchaguzi huo, Ghaib Lingo alisema kuwa katika
matokeo hayo Mbwana alichaguliwa baada ya kupata kura 39 na kumbwaga mpinzani
wake, Abdalah Rajab Abdalah aliyepata kura 16.
Kwa upande wa nafasi ya makamu Mwenyekiti wa Halmashauri
hiyo, Mfaume Wadali Halifa (CCM) alipata nafasi hiyo kwa kura 39 na kumbwaga
mpinzani wake Alliasa Mohamed Mshamu kutoka Chama Cha Wananchi (CUF) aliyepata
kura 16.
.
Wakitoa neno la shukrani kwa nyakati tofauti Mwenyekiti huyo
wa Halmashauri ya Tunduru, Mbwana Mkwanda Sudi na Makamu wake, Mfaume Wadali
waliahidi kutoa ushirikiano kwa madiwani na wataalamu wote katika kuhakikisha kwamba
wilaya hiyo inasonga mbele kimaendeleo.
Katika utekelezaji wa shughuli zao za usimamizi wa maendeleo,
walisema hawatakuwa na ubaguzi wala upendeleo wa aina yeyote ile kwani kufanya
hivyo wanaamini watajenga makundi yasiyokuwa ya lazima ndani ya wilaya, na
kuleta mipasuko miongoni mwa jamii.
Akizungumza katika mkutano huo wa kuzindua baraza hilo la
Madiwani, Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu aliwaasa madiwani ambao
waliingia katika baraza hilo kwa tamaa ya kutaka kupata fedha, kwamba safari
hii hakuna fedha na wanachotakiwa ni kuwatumikia wananchi.
"Kama wapo viongozi ambao wamepata udiwani kwa lengo la
kutekeleza vitendo vyao vya uporaji, ulafi na wizi wa fedha serikali ya awamu ya
tano chini ya Dokta John Magufuli hawatapata nafasi ya kufanya vitendo hivi",
alisema Mwambungu.
No comments:
Post a Comment