Na Steven Augustino,
Tunduru.
MBUNGE wa viti maalum, Zubeda Hassan kupitia tiketi ya Chama
Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alishindwa kuhudhuria kikao cha kwanza
cha kuwaapisha Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,
kutokana na Mbunge huyo kutofika na barua ya utambulisho kutoka makao makuu ya
chama hicho.
Msimamizi wa uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya
hiyo, Ghaib Lingo alitoa ufafanuzi huo mbele ya Madiwani wote wa wilaya hiyo,
ambao walihudhuria katika kikao hicho.
Akifafanua taarifa hiyo, alisema hali hiyo imekuja kwa lengo
la kutaka kujiridhisha juu ya uhalali wa kuteuliwa kwake na chama chake na
hawatambui kuwa ni Mbunge wa jimbo gani, kati ya Tunduru Kaskazini au Kusini.
Aidha aliwatoa hofu kuwa, Mbunge huyo ambaye pia serikali
inaamini kuwa ameteuliwa kihalali, atatambulishwa kwa Madiwani hao katika vikao
vijavyo mpaka barua yake ya utambulisho itakapowasilishwa katika Halmashauri
hiyo.
Katika mchakato wa uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka
huu, jumla ya vyama vitatu vilisimamisha wagombea wake wa ubunge katika wilaya
ya Tunduru mkoani Ruvuma.
Lingo alivitaja vyama vilivyosimamisha wagombea wa nafasi
hiyo, ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama Cha Wananchi (CUF) kupitia Umoja
wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na chama cha ACT Wazalendo.
No comments:
Post a Comment