Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, mgombea mmoja wa nafasi ya
Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, ambaye pia ni Katibu
wa siasa na uenezi mkoani humo, Benedict Ngwenya amewaacha hoi wanachama wenzake
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mbinga mkoani humo, baada ya kutokomea
kusikojulikana ikiwa ni lengo la kukwepa aibu na kusikiliza matokeo ya nafasi
hiyo aliyogombea.
Mwandishi wa habari hizi ambaye alishuhudia tukio hilo,
katika Ofisi za CCM wilaya zilizopo mjini hapa, Ngwenya licha ya kuombwa na
wanachama wenzake asiondoke katika eneo hilo hakuweza kuvumilia badala yake alipomaliza kupiga kura, aliingia kwenye gari gari lake na kuondoka.
Wakihojiwa na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti juu
ya hali hiyo, Madiwani wenzake wa Chama hicho walisema kukimbia huko anakwepa aibu
ya matokeo ya nafasi hiyo aliyogombea, ambayo awali alikuwa akitamba mtaani na
kujipa nafasi kubwa ya ushindi.
Benedict Ngwenya. |
“Sisi tumemshangaa sana, sote tuliambiwa hapa tusiondoke
mpaka taratibu za uchaguzi zikamilike, lakini mwenzetu alipomaliza tu kupiga kura tulimuona akiaga ghafla
na kuondoka huku akisema anasumbuliwa na tumbo”,
walisema.
Ngwenya ambaye pia ni Diwani wa kata ya Mpepai katika
Halmashauri ya mji huo, alipotafutwa kwa njia ya simu na mwandishi wetu, ili
aweze kuthibitisha hilo ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa.
Madiwani hao wa wilaya ya Mbinga kupitia tiketi ya Chama Cha
Mapinduzi, leo wamefanya uchaguzi wao ndani ya chama hicho na kuwateua wenyeviti watakaoweza
kuongoza Halmashauri zao, kwa kipindi
cha miaka mitano.
Uchaguzi huo umeendeshwa kwa amani na utulivu, tofauti na chaguzi
nyingine zilizopita ambapo kulikuwa na vurugu za hapa na pale huku ikifikia
hatua baadhi ya wafuasi wa chama hicho, kuchoma moto Ofisi ya Katibu wa CCM
wilaya.
Katibu wa Uchumi na fedha mkoa wa Ruvuma, Slim Mohamed ambaye
alikuwa msimamizi wa uchaguzi huo ametangaza matokeo majira ya mchana katika ukumbi
wa Chama Cha Mapinduzi, uliopo mjini hapa ambako chaguzi hizo zilikuwa
zikiendeshwa.
Uchaguzi huo ulikuwa ukifanyika kwa Halmashauri ya mji wa
Mbinga na ile ya wilaya ya Mbinga vijijini.
Kwa upande wa Halmashauri ya mji wa Mbinga, nafasi ya
Mwenyekiti na idadi ya kura walizopata katika mabano, imechukuliwa na Ndunguru
Kipwele ambaye ni Diwani wa kata ya Myangayanga aliyepata kura (15) na Makamu
wake ikichukuliwa na Tasilo Ndunguru, Diwani wa kata ya Kikolo kwa kura (17).
Kipwele katika nafasi hiyo aliweza kuwa bwaga chini Katibu wa
siasa na uenezi mkoa wa Ruvuma, Benedict Ngwenya ambaye pia ni Diwani wa kata
ya Mpepai aliyepata kura (7) na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mbinga ambaye ni Diwani
wa kata ya Kagugu, Christantus Mbunda (1).
Pamoja na mambo mengine, Tasilo naye aliweza kuwa garagaza chini
wapinzani wake ambao ni Aurelia Ntani kata ya Mbinga mjini ‘A’ aliyepata kura
(2) na wa viti maalum tarafa ya Mbinga mjini, Imelda Mapunda kwa kura (3).
Vilevile kwa upande wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga
vijijini, Mtarazaki Nchimbi kutoka kata ya Amani Makolo aliibuka mshindi kwa nafasi
ya Mwenyekiti akipata kura (22) akifuatiwa na Makamu wake, Benard Komba kutoka
kata ya Matiri aliyeweza kupata kura (22).
Mtarazaki alikuwa akipambana na wapinzani wake wawili, ambao
ni Winfrid Kapinga ambaye alijitoa dakika za mwisho katika kinyang’anyiro hicho
na Isaack Ndunguru aliyepata kura (16) huku Komba naye akiwaangusha chini Diwani
wa kata ya Kigonsera, Zena Mijinga (5) na Joackimu Kowelo kutoka kata ya
Mikalanga aliyeambulia kura (11).
Hata hivyo baada ya chaguzi hizo ndani ya chama kufanyika na
kuwapata Wenyeviti hao wateule, ratiba kamili ya kuwapeleka katika vikao vya
baraza la Madiwani na kufanyika uchaguzi wa kuwathibitisha kuwa wenyeviti
kamili, itatolewa wakati wowote kuanzia sasa.
No comments:
Post a Comment