Wanachama wa Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wakishiriki katika zoezi la kufanya usafi. |
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
WANACHAMA wa Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi (UVCCM)
wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamesema wataendelea kuunga mkono jukumu la
kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya mji wa Mbinga, ili kuweza kuepukana
na magonjwa yatokanayo na uchafu.
Aidha walieleza kuwa katika kuhakikisha kwamba jambo hilo
linakuwa endelevu ndani ya mji huo, watahamasisha watu wengine kufanya hivyo na
ni wajibu kwa kila mtu kuzingatia usafi katika eneo analoishi na sio kutupa
taka hovyo.
Wanachama wa UVCCM wilayani humo, walisema hayo walipokuwa
wakihojiwa na mwandishi wa habari hizi wakati walipokuwa wakifanya usafi
kuzunguka Ofisi za CCM wilaya na maeneo mengine, ya uwanja wa mpira wa miguu
ambao humilikiwa na chama hicho.
“Jukumu la usafi ni letu sote wananchi, sisi vijana
tumeungana kwa pamoja kufanya kazi hii katika eneo hili, tunawaomba wananchi
wengine watekeleze kwa vitendo suala hili ambalo ni muhimu mbele ya maisha yetu
ya kila siku”, walisema.
Awali Katibu wa Umoja huo wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi
wilayani Mbinga, Ally Simba ambaye alikuwa akiongoza kundi hilo la vijana
kufanya usafi wa mazingira katika maeneo hayo, alisema kwamba wanamuunga mkono
Rais John Magufuli kwa utendaji mzuri wa kazi ndani ya CCM ambao ameuonesha kwa
kauli mbiu yake ya ‘hapa kazi tu’.
Simba alisema kuna kila sababu, kwa kila mtu kutekeleza
majukumu muhimu ambayo yanaleta manufaa katika jamii kwa faida ya kizazi cha
sasa na kijacho ikiwemo suala hilo la usafi, ambalo linapaswa kuzingatiwa kila
siku.
Pia akielezea juu ya mikakati ya UVCCM wilayani Mbinga, alisema
wanachama wa umoja huo wanapaswa kujenga ushirikiano wa pamoja na kuacha
makundi yasiyokuwa ya lazima, ambayo yanaweza kuwagawa baadaye.
Hata hivyo aliongeza kuwa, mikakati mojawapo ya kuimarisha umoja
wao ni kujenga ubunifu wa miradi ya kimaendeleo na kuendeleza iliyopo, kwa
faida ya Chama na wanachama kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment