Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
BAADHI ya wananchi wanaoishi katika Jimbo la Mbinga mjini
mkoani Ruvuma, wamelalamikia juu ya kero wanazozipata katika Hospitali ya
wilaya ya Mbinga mkoani humo, ikiwemo baadhi ya waganga kuwa na tabia ya kuomba rushwa
kutoka kwa wagonjwa wanaokwenda hospitalini hapo kwa ajili ya kupata matibabu.
Rais John Pombe Magufuli. |
Aidha imedaiwa kuwa kundi kubwa linaloathirika wanapokuwa
katika hospitali hiyo ni la watoto wadogo na akina mama wajawazito, ambapo
wanapokuwa kwenye foleni kwa ajili ya kumuona daktari hukaa muda mrefu bila
kuhudumiwa na kusababisha wakati mwingine, mgonjwa kupoteza maisha.
Hayo yalisemwa na wananchi hao leo, kwenye mkutano maalumu ambao
uliitishwa na Mbunge wa Jimbo hilo la Mbinga mjini, Sixtus Mapunda katika
ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.
Mkazi mmoja wa kitongoji cha Lusonga aliyejitambulisha kwa
jina la, Gerwada Nchimbi alieleza kuwa hata mama mjamzito ambaye amejifungua
kwa njia ya operesheni endapo asipotoa rushwa ya fedha, dawa za kusafishia
kidonda hapati na anaambiwa akanunue kwenye duka la dawa muhimu ndipo
ahudumiwe.
“Mheshimiwa Mbunge, hata siku ya mwisho mama huyu anapotakiwa
kufungua nyuzi za kidonda chake hawezi kupata huduma mpaka atoe kitu kidogo kwa
mganga anayemkuta siku hiyo, tunaomba shughulikia haya ili tuweze kundokana na
kero hizi”, alisema Nchimbi.
Naye Rose Ndunguru mkazi wa mjini hapa, aliongeza kuwa hata
kwa upande wa wodi ya watoto, waganga wanaokuwa zamu wamekuwa wakitoa lugha
mbaya kwa wagonjwa na wauguzi wao ambao wamelazwa katika hospitali hiyo ya
wilaya ya Mbinga.
“Sisi tumechoshwa na hali hii, hawa watumishi wa idara ya
afya hivi hawaridhiki na mishahara wanayopata, sisi wanyonge tunaonewa sana
muda mwingine tukishapatiwa matibabu na mganga tunaambiwa………….wewe mama bado
unadaiwa hela ya soda”, alisema Ndunguru.
Kwa upande wake akitolea ufafanuzi juu ya kero hizo, Mbunge
wa Jimbo la Mbinga mjini, Mapunda alisema kuwa atakwenda kuonana na uongozi
husika na kuona namna gani matatizo hayo yanatafutiwa ufumbuzi ili yasiendelee
kuwepo.
“Ndugu zangu kweli Mbinga tunachangamoto kubwa juu ya
hospitali yetu, tunahitaji pia kuwepo na vifaa tiba na madawa ya kutosha,
tunahitaji kuendelea kushirikiana ili tuweze kumaliza matatizo haya yaliyopo”,
alisisitiza Mbunge huyo.
No comments:
Post a Comment